Moshi. Katika hali isiyo ya kawaida, mwanamme mmoja mkazi wa
Kijiji cha Kiria, Kata ya Mamba Kusini, Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro,
anadaiwa kuwabaka na kuwaingilia kinyume cha maumbile watoto wake wawili wenye
umri wa miaka 10 na 13 na kuwajeruhi vibaya.
Mwandishi alivyofuatilia
Ni saa 7:30 mchana nafika nyumbani kwa mwanamme huyo anayetajwa na baadhi ya
watu hapa Moshi kwamba anawabaka watoto wake.Nabisha hodi, sipati wa kunijibu,
baadaye anatokea jirani na kuniambia wenyewe hawapo, namweleza kilichonileta na
anakuwa tayari kunisaidia.
Jirani huyo ananipeleka kwa msamaria mwema anayemtunza mtoto wa miaka 13
aliyefanyiwa ukatili na baba yake mzazi kwa kubakwa na kulawitiwa kwa zaidi ya
miaka miwili na nusu sasa nikiwa njiani anasema “Unapomwangalia mtoto huyo
huwezi amini kuwa kitendo hiki kimetendwa na baba mzazi ambaye bila shaka kabla
ya kuwa na watoto aliomba kwa Mungu na alitamani sana kuwa na watoto naye aitwe
baba
Nafika kwa msamaria huyo katika Kijiji cha Kiria, Kata ya Mamba Kusini,
najitambulisha na kumweleza lengo langu, ananyanyuka na kuingia ndani kuzungumza
na mtoto anarudi na jibu lililonipa uchungu na kunitoa machozi. Anamtaja mtoto
jina na kusema amesema hataki kuongea na mwanamme, kama unataka mwambie huyo
mwanamme atoke hapo nje. Mwanaume anayezungumziwa ni yule ambaye alinisindikiza
kuja hapo kumwona.
Ilinilazimu nimwambie mtu huyo niliyekuwa naye aondoke ili nipate
nilichofuata kijijini hapo.
Baada ya kuondoka, mtoto huyo akiwa na uso wa majonzi alitoka nje na
kunisalimia kisha kukaa na kuanza kunieleza mateso na ukatili wa kutisha
aliofanyiwa na baba yake mzazi.
Mateso kutoka kwa baba
Mtoto huyo anasema hakumbuki siku ambayo baba yake alianza kumbaka lakini
anasema ni siku nyingi; mara baada ya baba yake kutengana na mama yao, zaidi ya
miaka miwili iliyopita.
Anasema baba yake huyo alianza kufanya unyama huo kwa mdogo wake ambaye sasa
ana miaka kumi na baadaye akaanza kumwingia na yeye na kwamba alikuwa akifanya
kwa zamu huku akiwafunga midomo ili wasipige kelele.
Anasema mara zote alipowafanyia unyama huo alikuwa na panga pembeni
akiwatishia kuwachinja kama watakataa au kusema kwa mtu yeyote.
Mtoto huyo anaeleza kuwa baba yao alioa mke mwingine, lakini bado akawa
anawaingilia, ndipo siku moja mwanamke huyo alipomfumania na kupigana nae sana
kabla ya kuamua kuondoka na kuachana naye.
(Source:Gazeti Mwananchi)
(Source:Gazeti Mwananchi)
No comments: