Serikali ya China imemtoza faini ya zaidi ya dola
milioni moja mtengeza filamu mashuhuri nchini humo, Zhang Yimou (pichani juu) kwa
kwenda kinyume na sera ya mtoto mmoja kwa kila familia nchini humo.
Bwana Zhang alikiri kuwa na watoto watatu na mkewe na ana hadi siku thelathini kulipa faini hiyo.China ilibuni sera ya mtoto mmoja mapema miaka ya sabini ili kudhibiti ongezeko la watu nchini humo.
Sera hiyo inashurutisha watu wanaoishi mijini kuwa tu na mtoto mmoja, ingawa familia za mashinani ziliruhisiwa kuwa na angalau watoto wawili ikiwa mtoto wao wa kwanza ni msichana.
Lakini mwaka jana, China iliamua kulegeza sera hiyo na kuruhusu familia kuweza kupata watoto wawili ikiwa mzazi mmoja wa mtoto huyo ni mtoto pekee kwao.
Faini hiyo ilijumlishwa kulingana na mapato ya bwana Zhang na mkewe Chen Ting, wakati watoto wao wawili walipozaliwa.
Wawili hao walipata mapato ya dola $580,000 mnamo mwaka 2000, 2003 na 2005 kwa mujibu wa serikali.
Mkewe Zhang hata hivyo amekanusha madai kuwa mumewe alipata watoto wengine na wanawake wa kando .
Zhang, mwenye umri wa miaka 61, alitengeza filamu maarufu za China ikiwemo, Hero, The House of Flying Daggers pamoja na The Flowers of War.
(Picha na habari kwa hisani ya BBC Swahili)
No comments: