Latest News


More

MADHARA YA KUYAPA KISOGO MASOMO YA DINI SHULENI

Posted by : Unknown on : Monday, January 20, 2014 0 comments
Unknown

Wazazi, walimu, viongozi na jamii kwa jumla kila mmoja analia kuhusu kuongezeka kwa mmomonyoko wa maadili nchini.
Waathirika wakubwa wa kadhia hii ni vijana wakiwamo wanafunzi katika madaraja mbalimbali ya elimu. Mathalani siyo ajabu leo kusikia wanafunzi shuleni na vyuoni wanavuta bangi, walevi au wanajihusisha na vitendo viovu vya ngono. Nyumbani na mitaani nako siyo shwari, vijana wametopea katika kufanya mambo yaliyo kinyume na maadili ya Kitanzania na hata utu kwa jumla.
Chanzo cha tatizo
Ilivyo ni kuwa mafundisho ya dini yamewekwa kando. Kibaya zaidi fursa za kuwafunda vijana kupitia masomo ya dini shuleni, nayo haipewi msisitizo kama ilivyo kwa masomo mengine.
Baadhi ya watu wanashangaa Serikali kutokuwa mstari wa mbele kupigania ufundishaji imara wa masomo ya dini, hatua wanayosema ingesaidia kupunguza matukio mabaya yanayoipa Serikali wakati mgumu kupambana nayo.
“ Serikali haionekani kama inayatilia maanani masomo haya, ndiyo maana imeyafanya kuwa ya hiari. Wasichokijua viongozi wetu ni kuwa matatizo wanayosema yanaisumbua Serikali kama vile uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya ni matunda ya watoto kutopewa misingi ya dini zao kupitia mafundisho,’’ anasema mkazi wa Dar es Salaam, Thobias Mnomole na kuongeza:
“Hii ni ajabu badala ya Serikali kuyapa kipaumbele, leo Serikali inasema masomo hayo hayatochangia katika ufaulu, yaani hata ukipata alama A ni sawa na bure tu. Huku ni kuwafanya wanafunzi wazidi kuyakimbia. Kwa nini wasiyafanye kuwa masomo ya lazima ili kizazi hiki kiokolewe?
Mnomole ambaye ni mzazi wa mtoto mmoja anaeleza kuwa hata kama uendeshaji wa Serikali hauzingatii dini, kwa Tanzania mafundisho ya dini bado yana umuhimu mkubwa kwa kuwa ndiyo njia pekee inayoweza kutumika kujenga kizazi bora, chenye amani na ambacho hakitoisumbua Serikali yenyewe.
Tatizo la jamii
Mzazi na mkazi wa Ilala jijini Dar es Salaam, Abdu Bakari anasema kupewa kisogo kwa masomo ya dini shuleni ni matokeo ya jamii kutoipa dini nafasi katika maisha.
Anasema Watanzania wengi wamejiweka kando na mafundisho ya dini, hivyo haishangazi hali hiyo kujiakisi pia katika mazingira ya shule.
“ Watendaji serikalini ambao ndiyo watunga sera na hata walimu shuleni ni zao la jamii hiyo hiyo isiyojali dini. Kwa hiyo nani sasa atayapa kipaumbele masomo ya dini?’’ anahoji.

No comments:

Leave a Reply