Latest News


More

HUDUMA YA UKOMBOZI WA FAMILIA NA MIJI

Posted by : Unknown on : Wednesday, May 22, 2013 0 comments
Unknown
Saved under : ,

Halleluya mtu wa Mungu, maana halleluya inawapasa wanyoofu wa moyo ambao ni mimi na wewe (Zab 33:1 b).

Ni mimi Mtumishi wa Mungu Israel Kisanga wa huduma ya OVERWOMEMI – International tukiwa sambamba na Tanzania Ebenezer Foundation/Ministry ambao kwa pamoja tumekuwa tukifanya kazi ambayo Kristo alitutuma ya kuwafungua watu katika vifungo vyao vya nafsi, Mwili, Roho pamoja na mazingira yanayotuzunguka.

Baada ya utambulisho huu, karibu sasa katika mwendelezo wa huduma ya Ukombozi wa Miji tulioufanya katika nyumba yako kwa njia ya ujenzi wa Madhabahu.

Lengo la maelezo haya tunayokupa ni kukuandaa kimaombi,maombi  ya mwendelezo wa huduma ya Madhabahu tuliyoijenga hapo nyumbani kwako.  Ninaamini kwamba mwisho wa maombi haya na yatakayoendelea kulingana na ufunuo tuliopewa na Bwana kupiti (matayo1:23b.Nao watamwita jina lake Imanuel;Yaani Mungu pamoja nasi).Tunahitaji hilo neno litimie kwako la Mungu kuwa pamoja na mji,familia na mazingira yako.

Safari ya somo letu la ujenzi wa madhabahu umeanzia mbali sana toka katika Ukombozi wa ardhi ambo chazo chake ni katika mwanzo (3:14 – 19) baada ya Anguko la Adamu. Tunaona ardhi ikilaaniwa maana yake ni uzima/uwepo wa Mungu ukiondoka katika ardhi/makazi na mauti ikitawala.

Kutokana na Anguko hili ambalo halikuwa katika mpango wa Mungu, kwa nyakati mbalimbali Mungu alionekana akijidhihirisha kupitia watu tofauti tofauti kwa nyakati mbalimbali kama vile Nuhu, Ibrahimu, Taifa la Israeli na mwishowe kupitia Kristo Yesu Bwana.

Kupita Nuhu na familia yake tunamwona Mungu akifunua ule mpango aliokuwa ameuweka Maishani mwa Adamu ya kumiliki na kutawala viumbe vyote (mwanzo 1:26-28), Pia tunaona Mungu akibatilisha laana na kurejesha majira na nyakati katika Nchi (ardhi) (Mwanzo 8:21– 22,).

Agano ambalo Mungu aliliweka kupitia Nuhu, halikuishia kwa Nuhu na watoto wake ila pia uzao utakao kuja baada yao (mwanzo 9:8-12), wanyama, ndege, pamoja na Nchi (ardhi).

Kwa upande wa Ibrahimu, yeye pia tunajifunza mambo kadha wa kadha, jambo la muhimu tutakalo lichukuwa kwake ni lile la ujenzi wa madhahabu katika kila eneo ambalo aliweka hema/makazi /Nyumba yake Mwanzo 12:7-8).

Wapendwa, naomba niwakumbushe maana ya Madhahabu.Madhabahu ni mahali (Kutoka25:8)/eneo/nafasi/makazi /msakani/nyumba  (mwanzo28:17)ambayo Mungu anakaa. 

Kwa maana nyingine, Madhabahu inawakilisha uwepo wa Mungu/Miungu fulani katika eneo walilotengewa.

Hivyo madhabahu zinawakilisha uwepo wa Mungu hapa duniani anayeishi/kaa katika Ulimwengu wa Roho

Madhabahu ni Nyumba  /Nyumba/kiti (ufunuo2:13)/makazi/eneo/anapoishi Mungu.

Sasa kwa kuwa madhabahu ni Nyumba /makazi/ eneo/ maskani ya Mungu, inapojengwa nyumbani Mwako/ kwenye makazi yako/mji wako kinachotokea ni kwamba Mungu aliyejengewa hiyo madhabahu anatoka katika ulimwengu wa Roho na kuja kuweka/ Kuishi na wewe katika mji wako/nyumba/familia yako.

     Hivyo hiyo Madhabahu inakuwa ni ishara ya uwepo wa Mungu katika mji wako na Mungu anajifunua kupitia hiyo madhabahu.

     Baada ya kupata maana halisi ya madhabahu basi utafahamu kwamba Ibrahimu alitambua umuhimu wa Mungu wake kuishi naye  katika kila mahali alipokwenda lengo ni kwamba alitambua umuhimu wa uwepo wa Mungu katika maisha yake ya kila siku, lakini pia alijua siri ya yeye kufanikiwa katiki ulimwengu huu wa mwili na nyama unaaza katika ulimwengu wa Roho hivyo ni lazima auvute ulimwengu wa Roho ambao umekamilika kwa kila kitu uje uishi hapa duniani ambapo pana mapungufu ya kila namna.

     Naomba nikufahamishe kwamba hakuna namna tutakavyoweza kuishi hapa duniani kwa mafanikio na maisha yenye ushuhuda tena ya ushindi kama hatutakuwa na mfungamano na ulimwengu wa Roho wa Mungu aliye hai.

     Njia itakayokuunganisha wewe uliyeko katika  Ulimwengu wa mwili (dunia) na ulimwengu wa roho (mbingu) ni madhabahu.

Mahusiano kati ya mtu aliyeko hapa duniani na Mungu aliyeko Mbinguni yanajengwa kwa kupitia Madhabahu.

Katika kitabu cha kutoka 25:1 –8, ili Mungu apate kuishi katikati ya wana wa Israel aliwaagiza wamfanyie patakatifu. Maana yake wamtengee mahali/wamjengee nyumba/wamtengenezee kiti cha yeye kuketi/kutawala juu ya Israel wote.

Alichokuwa anakitaka ni Madhabahu ili aje akae nao na kuishi nao katika  maisha ya kila siku.

Tumekwisha kuwatazama Makundi ya watu wa aina tatu. Makundi mawili yanatabia zinazofanana ambayo ni Nuhu na familia yake na Ibarahimu na uzao wake.

Tumekwisha kuwatazama makundi  ya watu  wa aina tatu.Makundi mawili yanatabia zinazofanana. Ambayo ni Nuhu  na familia yake pamoja na Ibrahimu na nyumba yake na kundi la pili ni Taifa la Israel.

 Katika kundi la kwanza madhabahu zote walizozifanya ziligusa familia/ndoa na watu, pamoja na maendeleo yao ya kila siku.

Hawakujenga kwa nia ya huduma au kisiasa bali ni kwa ajili ya miji na maisha yao  ya kifamilia.Makundi haya mawili ndio yatakayokuwa msingi wa maombi yetu kwani madhahabu zile tulizozijenga, tulizijenga katika mji/makazi/nyumba/zetu, lengo likiwa ni kwamba Mungu aliye mbinguni aje aweke makazi katika familia na miji yetu.

Kwamba tulijifunza aina tatu za Madhahabu wakati wa ujenzi. Tulisema kuna madhahabu ya udongo kutoka 20:24, Madhahabu ya mawe kutoka 24:4 na Madhahabu ya mti ambayo tunaipata katika kitabu cha kutoka 27: 1 – 8.

Madhahabu tuliyoichukuwa ni ile ya mti inayotasfirika katika Agano jipya kama Msalaba wa Kalvari (Yesu).

Hii Madhahabu ndiyo tunayotembea nayo na ndiyo msingi wa maombi yetu tuliyoyafanya kwako.

Kumbuka pia kwamba katika Msalaba wa Yesu tuliona mambo manne ambayo yalitolewa/yalipelekwa hapo kama dhabibu na Yesu mwenyewe. Mambo hayo ni:

1.      Mwili wake ambao kwetu uliwakilishwa na Biblia/Neno takatifu (Yohana 1:14)

2.      Damu yake  ambayo sisi iliwakilishwa na uzao wa Mzabibu (Luka 22:14 – 20) (Yohana 19:34)

3.      Maji ambayo kwetu tuliwakilishwa na chupa 12 za maji (Yohana 19:34) (Yohana 4:10 –14) Wafalme18:33 – 35.

4.      Roho wake – ambao sisi tuliwakilishwa na chupa saba za mafuta (Isaya 11:2 – 3)

 

Rejea katika zaburi 50:5 ambao wanasema “Nikusanyieni wacha Mungu wangu waliofanya Agano/(walionijenga Madhabahu) kwa njia ya sadaka/dhabibu.

     Hapa ningetaka ujue kwamba kila kinachotolewa madhabahuni ni sadaka/na pia sadaka hizo hugeuka kuwa Agano kati ya aliyetoa na aliyepokea.

     Kwa tafsiri hii tutakubalia kwamba Bwana Yesu alipeleka pale Msalabani (katika Madhabahu yake aliyomjengea Mungu (madhabahu 27:1-8) dhabibu za aina nne ambazo zote kwa pamoja zinanenwa kuwa toleo moja lidumulo hata milele (Hebania 10:12 – 13. Lakini huyu alipokwisha kutoa dhabihu moja idumuyo  hata  milele, aliketi mkono wa kuume  wa Mungu;).

     Kama matolea/sadaka /dhabibu hugeuka na kuwa Agano, basi ndani ya hizi sadaka nne ambazo ni maji, damu, mwili na roho tutapata agano la maji, Agano la Damu, Agano katika mwili wake na Agano katika roho wake.

    
Hivyo Agano jipya limejengwa na maagano madogo madogo manne ambayo ni:

·         Agano katika damu yake Luka 22:14 – 20

·         Agano katika Mwili wake Luka 22:14 – 20, Yohana 6:49 – 59

·         Agano katika maji yaliyotoka mwilini mwake Yohana 19:34, Yohana 4:10 – 14.

·         Agano katika roho wake Isaya 11:2 – 3. Isaya 59:21.

 

     Haya ni maagano manne yahayotengeneza Agano jipya ambalo Yesu Kristo alilifanya pale Kalvari kwa ajili ya ulimwengu wote.

     Ninaamini kwamba umenielewa kwa mafafanuzi hayo hapo juu kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

      Agano la Maji ya uzima.

     Yohana 4:10 – 14 Baadaya mwanamke msamaria kukutana na Bwana Yesu, tunamwona Bwana yesu akimwambia ''Kama ungejua karama ya Mungu naye ni nani akuambiaye Nipe maji ninywe,ungelimwomba naye angalikupa   maji yaliyo hai.Kama kuna maji  ambayo hayakuwepo ulimwenguni  ni yale   ambayo Yesu/Mungu aliyatoa katika mwili wake. Baada ya kifo chake pale msalabani tuna mwona Askari mmoja akienda na kumchoma mkuki ubavuni. ''Lakini askari mmoja wapo alimchoma ubavu kwa mkuki na mara ikatoka damu na maji'' (Yohana 19: 34).

     Haya ndio yale maji ambayo Yesu alikuwa ameyabeba  yaliyo kuwa yamebeba uzima.

     Uzima ni zaidi ya uhai , mtu anaweza kuwa hai lakini asiwe na uzima katika eneo fulani la mwili wake.

Hivyo uzima ni ile hali ya ustawi/ufanisi/kufanikiwa/afya bora/kuongezeka (Yeremia 17:5 – 10). Vifungu hivi vinaelezea jinsi makundi ya watu wawili wanavyoonekana kimaisha.

Kundi la kwanza ni la mtu aliyeko katika laana na matokeo ya maisha yake ambayo ni:

·         Ufukara

·         Maisha ya ukame

·         Ukiwa /mahama

·         Uduni /udhaifu n.k

     Haya maisha ni maisha ya mtu aliye kata tamaa kabisa, ni miji iliyosambaratika kabisa. Miji iliyokufa imebaki kuwa magofu, watu wameicha, hapafai kuishi, maana yake kila kinachofanyika hapa badala ya kuongezeka vinapukutika na baadaye kufa. Kama ni wanyama wa kufugwa wanakufa, au hawazai,au wanazaa na watoto wanakufa, ndoa zinavurugika,watu hawapati mimba,ukiweka mradi unakufa au unakupelekea hasara,magonjwa ya mara kwa mara na hali kama hizo.

     Kundi la pili ni kundi la watu waliobarikiwa. Kundi hili limefananishwa na mti ambao umepandwa kando ya maji. Kutokana na uwepo wa maji maisha ya ule mti yalikuwa ni mazuri yenye kupendeza, ulizaa matunda mazuri na ukawa kama eneo la kusitiri watu kwa kivuli chake wasipigwe na jua.

     Hivyo tumeona maji yanavyoweza kubadilisha hali ya mmea na kuupelekea katika maisha mengine kabisa.

     Kitendo cha Yesu kutuletea maji pale msalabani alikuwa hatuletei tu maji bali uzima utakao badilisha maisha yetu.

     Ndiyo maana aliyatoa yale maji ubavuni ili yakabatilishe yale maisha ya laana ambayo ilikuwa ikitembea juu ya ardhi na katika maisha yetu.

     Agano hili la maji ya uzima/ Baraka linapotembea katika maisha yetu,linageuza  hali  ya maisha yetu kutoka katika kundi la yule mtu aliyekuwa amefungwa kwenye kifungo gereza la laana na kutuingiza katika maisha ya uzima ambapo ni mahali pale ambapo Adamu wa kwanza alikuwa anaishi, mazingira yale yaliyokuwa yanaonekana katika ile bustani ya edeni kabla ya anguko.

     Bustani ya edeni likuwa ni mazingira mazuri ya kupendeza ambapo Mungu alimwekea Adamu kuwa makazi yake ya kuishi.

     Tukiangalia bustani ya Edeni tunaiona ikiwa na mto ambao ulikuwa umegawanyika vipande vinne kila kimoja kikielekea upande fulani na hivyo kutengeneza pande nne za dunia ambapo ni Kaskazini, Kusini,Mashariki na Magharibi.( Mwanzo 2:10 – 15)

Tena ukiangalia mji wa Yesulemu ule mpya ambapo ndipo tunapokwenda kuweka makazi yetu ya umilele, umezungukwa pande nne za dunia na malango kumi na mbili ambayo Kaskazini kuna mlango matatu, Kusini matatu, Mashariki matatu na Magharibi pia matatu.

     Huu ni mji mpya ambao sisi tuliookoka tutakwenda kuishi. Ni mahali pazuri penye nuru inayo angaza maasa yote na hakuna usiku mahali hapo. Tunaweza kusema ni eneo lililojawa na uzima/uwepo wa Mungu.

     Tuliposimama na maji chupa 12, tulimaanisha kwamba kila moja inawakilisha toleo la maji ya uzima. Agano la uzima linasimama kwa kila kabila moja.

     Maana nyingine ni kwamba kila chupa iliwakilisha toleo dhidi ya kila kabila/mlango ambayo yanatengeneza  Taifa la Israel na  ambayo jumla yake ni 12.

     Tunachotaka kitokee ni malango 12 ambayo ni makabila 12, kupitisha uzima kuja katika mji wetu.

     Mji wako unasimama badala  ya mji wa Yerusalemu (mpya) (ufunuo 21: 1-8)na yale malango yake ni yale mawe 12 ambayo tuliyatumia katika kujenga madhabahu, na hizo chupa 12 za maji ni Agano la uzima dhidi ya kila mlango/kabila.

     Hatutaki tena mauti/laana kuingia na kutawala juu ya mji/nyumba/familia  yako,tunataka uanze kuishi maisha  ya umilele/Yerusalemu mpya hapa duniani kwa muda huu ambao Mungu amekupa.

     Tunaivuta Yerusalemu mpya katika maisha yako kuja kaika wakati wa  sasa kwa imani(waebrania 11:1) na unaanza kufaidi mambo ya baadae wakati ,huku ukisubiri wakati  wa kwenda katika ule mji halisi wa Yerusalemu.

     Naomba nikurudishe nyuma kidogo idadi ya chupa kumi na mbili tunaipata katika Agano la kale katika 1waflme18:33-34) ambapo Nabii Elia alimjengea Mungu Madhabahu na baada ya matoleo yale matatu ambayo ni mwli,damu na roho ya yule ng'ombe, aliagiza toleo lingine la nne  ambalo lilikuwa ni la maji mapipa 12 (kumi na mbili) juu ya madhabahu. Hapa ndipo palipotupa namba 12 ya maji ambayo tunatembea nayo katika ufunuo huu.

     Mahusiano kati ya Mungu na maji na Ibilisi na maji

     Katika Kitabu cha Mwanzo 1:2 – 3 tunamwona Roho wa Mungu akiwa juu ya vilindi vya maji maana ya neno juu kiroho linamaanisha utawala dhidi ya kitu kingine.

     Hivyo Roho wa Mungu alikuwa ameketi/anatawala juu ya vilindi vya maji. Ufunuo 17:1 -5 hapa tunamwona Yezebeli ambaye katika ufunuo 13:1-10 amenenwa kama mnyama aliyetoka katika maji. Tena inamwelezea uwezo wake mkubwa aliokuwa nao na jinsi alivyotenda mambo ya ajabu.

     Mwanamke huyo aitwaye Yezebeli (Ufunuo 17: 1 – 6) anaonekana akiwa na vichwa saba ambavyo kwa upande wa Kristo tuna wakilishwa na Roho saba za Mungu.

     Pia ameonekana na  pembe 10, Ufunuo 13:1 – 10, ufunuo 17:3, ambazo ziko juu yake na pembe nyingine mbili zilikuwa juu ya yule mnyama aliye toka katika nchi (ardhi) ufunuo 13:11 – 18.

     Ukichukuwa pembe 10 za yule mwanamke na mbili za yule mnyama aliyetoka katika ardhi/nchi zinatupa namba 12, idadi ya makabila/malango 12  ya Taifa la  Israel.

Hizo pembe  ni mamlaka/falme/nguvu/uwezo/malango 12 ambazo ibilisi  anayatumia  katika ufalme wake  kama  vile Yesu alivyo na Makabila 12 yayopisha  na kusimamisha ufalme wake wa Mbingini.

     Mnyama aliyetoka katika nchi/ardhi alikuwa na pambe mbili ambazo zinawakilsha falme/mamlaka/roho/uwezo/ mbili zinazotawala juu ya ardhi.Kuna nguvu/falme mbili za kuzimu zinazotawala juu ya ardhi.

    

     Pembe kumi zilizokuwa juu ya Yule mwanamke ni mamlaka/falme/idara 10 za kuzimu zilizoko chini ya Yezebeli zinzotawala juu ya maji/watu.

     Kumbuka huyo anavyo vichwa saba (falme 7) pia anazo pembe 10 zote hizi ni Mamlaka na uwezo wa kipepo unaotenda kazi ndani ya roho ya Yezebeli.

     Maji Kibiblia yana maanisha watu wengi, hivyo kuna mapepo/ roho saba ambazo zinaishi au tawala ndani au juu ya mtu/maisha yake, ambzo ni nguvu ya kiyezebeli na pia zipo nyingine kumi Idara ambazo kazi yake ni kuhakikisha unaishi katika utumwa wa Ibilisi hata kama wewe hupendi.

     Katika ardhi zipo pembe mbili (2) ambazo ni mapepo/nguvu/falme mbili ambazo zinatawala ardhi na kuendesha utawala wa kuzimu katika mazingira tunayoishi. Hivyo Ibilisi ameweka utawala wake juu ya watu (maji) na juu ya nchi ambayo ni ardhi/mazingira yanayotuzunguka.

     Huyu mwanamkw alipewa uwezo mwingi sana 13:5 – 6 na uwezowa  kinywa chake kunena makufuru.
     Neno kufuru ni kitendo cha kufanya jambo lililo katika uwezo wa Mungu. (marko 2:1-6)''Katika kifungu hichi Yesu aliposema kwamba umesamehewa dhambi zako mafarisayo walisema huyu anakufuru kwa sababu hakuna mwanadamu mwenye uwezo wa kusamehe dhambi ila Mungu pekee''

     Yeye alipoonekana kana kwamba ni mtu wa kawaida, watu wote walikuwa wanamwona kama mwanadamu ila yeye hakuwa tu mwanadamu lakini pia Mungu kamili.(yohana 1:1).............naye neno alikuwa Mungu''

     Sasa aliposimama kama Mungu, wale waliokuwa wanamtambua kama mwanadamu, hawakumwelewa ndio maana wakawa wanaona kwamba Yesu Kristo anajifananisha na Mungu kitendo ambacho kwake yeye hakikuwa kujifananisha bali alikuwa Mungu kweli.

Marko3:22-23 Hapa tunaona kitendo cha Yesu akitoa pepo. Jambo hili la kumtoa mtu pepo lilileta mtafaruku kwa watu. ….Nao waandishi walioshuka kutoka yerusalem wakasema,Ana Beelzbuli, na, Kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo.Hivyo tunaona wakimfananisha/wakifananisha kazi ya utendaji wa Mungu aliye hai  na (Mkuu wa pepo)

     Baada ya maneno yao, Bwana Yesu akaanza kuwaeleza kwamba hayo maneno yenu ni makufuru kwa Mungu kwani kitendo cha kumfananisha Mungu/Yesu/Roho mtakatifu na mapepo au ibilisi au mojawapo ya idara yake  ni kukufuru.

     Hivyo kukufuru ni kujifanya wewe kuwa ni Mungu au ni kunena kinyume cha Yesu/Roho mtakatifu au kufanya jambo lolote linaloibeza kazi ya Mungu.

     Kama kukufuru ni kufanya yale ambayo ni Mungu pekee anayoyatenda ili wewe uonekane kuwa ni Mungu au uabudiwe ni dhahri kwamba vile vichwa saba ni ambavyo viko juu ya Yezebeli ni roho saba chafu za kuzimu zinazosimama mbadala wa Roho saba za Mungu.

     Kumbuka tuna Roho Saba za Mungu (Isaya 11:2 – 3) ambazo ni:

1.      Roho wa BWANA

2.      Roho wa Hekima 

3.      Roho wa ufahamu

4.      Roho wa uweza

5.      Roho wa shauri

6.      Roho wa maarifa

7.      Roho wa kumcha Bwana


     Hizi zipo katika upande wa Mungu aliye hai. Na hizo Roho saba ndizo zinazotengeneza  namba saba ambayo ni ukamilifu wa BWANA/Mungu.

     Sasa kama ibilisi ameweka makufuru, inamaana badala ya Roho wa bwana yeye amegeuza na kumweka belzebuli ambaye ndiye mkuu wa mapepo

·         Hekima -ameweka hekima ya dunia/kipepo.

·         Maarifa -ameweka pepo la ufahamu wa giza/dunia.

·         Uwezo   -Pepo la uwezo / upako/mamlaka ya kishetani/dunia.

·         Shauri   - pepo la mashauri ambayo hayatokani na Mungu yenye lengo la kupotosha watu waende nje ya mpango wa mungu.

·         Kumcha Bwana-hapa shetani amesimamisha pepo ambalo kazi yake ni kuhakikisha watu wanamtii/Mwabudu shetani/joka.

 

Namba kumi na mbili katika Kanisa inawakilishwa na majina kumi na mbili ya kabila la Israeli ambyo ni:

1.      Rubeni – Macho ya Mungu (mwanzo 29:32)

2.      Yuda – Ufalme/Utawala

3.      Lawi – Ibaada/ukuhani (mwanzo 29:34)

4.      Yusufu – Mamlaka juu ya ardhi

5.      Dani – Haki/hukumu (mwanzo 30:6)

6.      Benjamini – Nguvu za Kijeshi

7.      Asheri-Chakula/tunu/watoto/kibali/heri/baraka.( Mwanzo30::13,mwanzo49.20,kumbukumbu 33:24)

8.      Naftaili-Ushindi/utele/fadhili(mwanzo 30:8,kumbukumbu 33:23)

9.      Gadi -Mtoa sheria(kumbukumbu 33:21-22)

10.Isachari – Kazi/mapato/mshahara(mwanzo 30:14-18)

11.Zabloni  -Furaha/makazi/mahari(Mwanzo30:20,Kumbukumb 33:18

12.Simeoni – Kusikia/ masikio ya Bwana (mwanzo 29:33)

Kila kabila linapitisha maana Fulani katika Taifa la Israel. Hivyo kila kabila ni Idara/Pembe/mamlaka inayoratibisha maisha ya watu katika Taifa la Israel.

Sasa katika ufalme wa giza  yapo malango mawili ambayo  yanayotenda kazi kwa ajili ya kuthibitisha ufalme wa giza juu ya ardhi.

Hivyo mengine yote yapo chini ya Yezebeli ambapo uratibu wake  ni juu ya watu.


Baada ya mafafanuzi haya yote tunataka tuingie katika maombi.Tutakuwa na siku saba za kung'oa na kuharibu vile vichwa saba (mapepo saba) baadaye tutakuwa na siku nyingine saba za kupanda Roho saba za Mungu.Maombi haya

1.      Wiki ya kwanza siku saba(Yeremia 1:10 ) (Matayo 15:13)

Maombi yake ni kama ifuatavyo

Toba kwa familia:

Baba katika jina la Yesu ninakuja mbele zako kwa damu ya mwanao Yesu Kristo. Ninatambua maovu yangu yote ambayo nimekutenda wewe kwa kujua na kutokujua. Ninatubu kwa ajili ya mji wangu, Baba yangu, mama yangu, watoto wangu (taja wote kwa majina) mke wangu, mume wangu, mashangazi, wajomba, mama wadogo, mama wakubwa, mabinamu, wajukuu, na uzao wangu wote na watu wote wanonihusu kutoka upande wa baba na kutoka upande wa mama.

Toba kwa ajili ukoo:

Ninatubu pia kwa upande wa ukoo wangu maovu yao yote na yote waliokutenda yaliyokuchukiza mbele zako kwa sababu nimejua ya kuwa Yezebeli alipewa watu wa kila ukoo.Ninatubu kwa ajili ya waasisi wa ukoo wangu,viongozi wate waliopita na waliopo katika ukoo wangu,maovu yao,dhambi na machukizo waliyokutendea,maagano na makafara yote waliyofanya juu ya ukoo wetu na vizazi vyake.Naomba rehema zako na msamaha kwa ajili ya mambo yote tuliyoyatenda kama ukoo,kwa upande wa babu mzaa baba,bibi mzaa baba,babu mzaa mama na bibi mzaa mama yagu na koo zote tuliyofungamana kwa namna mbalimbali.

Toba kwa ajili kabila

Ninasimama pia na damu ya Yesu kwa ajili ya kabila langu. Ninawaleta wote kwako nakuomba Bwana utusamehe maovu na dhambi  ambazo waasisi na wahenga wa kale waliyoyatenda,ikiwa ni pamoja na maagano yote yaliyofanyika ,yaliyotuunganisha na ulimwaengu wa giza kwa njia mbalimbali ikiwemo mila na desturi na kila uchafu tulioufanya kupitia machifu na viongozi mbalimbali,ambazo katika hayo sisi kama familia tumejikuta tukiunganishwa  na kupalizwa japo sisi hatukutenda hayo sawa na kutoka 20:1-5

Toba kwa ajili ya Taifa.

Ninakuomba unisamehe na ulisamehe Taifa langu na watu wote  wa Tanzania  katika damu yako.Tumetenda dhambi sisi kama watanzani,wahenga wetu,waasisi wetu,viongozi mbalimbali na maagano yote yaliyotuunganisha na Yezebeli pamoja na kuzimu kwa ngazi ya kitaifa.

Ninajifunika mimi na damu yako, nafunika mji wangu na wote walioko ndani yake kwa damu ya yesu kabila langu na taifa langu lote pia ninalifunika kwa damu ya Yesu Kristo.

    Ninasimama na Agano la maji ya uzima sawa na Yohana 4:10 kung’oa, kuharibu na kuangamiza kabisa roho ya Yezebel na vichwa vyake saba ndani na juu ya maisha yangu. Ninasimama kinyume cha Yule mnyama aliye toka katika maji na vichwa vyake saba pamoja na matokeo ya utendaji wake na athari zake ndani yangu. Ninapeleka makombora ya maji ya uzima katika jina la yesu kristo,Ninampiga huyo mnyama napiga na kuharibu vichwa vyake vyote vile vilivyosimama mbadala wa Roho saba za Mungu katika maisha yangu zinazotembea katika mwili wangu, zinazotembea katika damu na mfumo wa maji ulioko katika miili yetu ambayo tumeridhi kutoka kwa baba na mama zetu sawa na 1 petro 1:18 – 24 na Ezekiel 16: 1 – 6.katika jina la Yesu Kristo tunaziangamiza kabisa hizo silka ambazo ni kutoka kwa baba zetu, leo tunaziangusha, tunabomoa, tunaziteketeza kabisa katika jina la Yesu ili tuweze kuishi na kutembea katika uhuru na maisha yale mapya uliyotupa kupitia msalaba wa Yesu. Ili sisi wanao, miji yetu, Nyumba zetu na familia zetu ziwe na ule uzima ulioutoa tena tuwe nao tele.

      Katika jina la Yesu Kristo ninaendelea kuharibu mfungamano wa hizo roho/mapepo/vichwa saba vya Yule Yezebeli pamoja na Yezebeli Mwenyewe, unaotokana na ukoo wangu/ zetu, kabila langu/letu, na Taifa letu kwa ujumla maana yule mnyama aliyetoka baharini alipewa watu wa kila kabila, koo/jamaa na Taifa (ufunuo 13:7) Hivyo ninasimama kinyume cha huyo mnyama katika ngazi ya ukoo, kabila na Kitaifa kwa mamlaka ya jina la Yesu Kupitia Agano hili la maji ya uzima. Ninaharibu maagano yote yanayotushikilia na tabia/silka/vichwa vyote saba vya ukoo, kabila,na kitaifa vinavyofuatilia maisha yetu na vinavyotawala,vile vichwa saba katika ngazi ya familia,vichwa saba katika ngazi ya ukoo,vichwa saba katika ngazi ya jamaa,vichwa saba katika ngazi ya kabila na vichwa saba katika ngazi ya taifa. Tunavipiga na kuviangamiza, tunaharibu na kuviteketeza kabisa katika jina la Yesu.

     Tunakuharibu belzebel mkuu wa mapepo, hekima za kipepo, maarifa ya kishetani, ufahamu wa kuzimu, mashauri na roho zote za kishauri za kipepo, uweza wa giza na roho zote zinazotupelekea kumcha shetani/ Yule joka (ibilisi) kwa mamlaka ya jina la Yesu kristo Wanazareti, wewe bwana ndiwe uliyesema na kanisa na kutuambia tuje tuone hukumu ya yule babel mama wa makahaba na machukizo ya nchi (ufunuo 17 :1 – 3, tena wewe ndiwe uliyewaanganiza wamisri, Farao na jeshi lake kwa maji ya bahari ya shamu wakati walipokuwa wanawafuatilia watu wako Israel baada ya kuwatoa katika utumwa kule misri.(kutoka 14:26-31)

       Hawa wamisri waliokuwa wanawafuatilia watu wako wanawakilisha utawala wa kichawi katika ulimwengu wa roho uliokuwa unatawala kule Misri na uliokuwa unawakandamiza watu wako Israel.

       Leo hii ninatangaza kwamba kwa mamlaka ya jina la Yesu kama vile wewe baba ulivyotenda kwa lile Kanisa la kwanza ni wakati wako sasa kutenda katika maisha, nyumba, familia, miji na uzao wetu.Katika jina la Yesu ninatangaza kwamba Yezebeli na vichwa vyako kwamba umeanguka vichwa vyako vimeanguka, falme zako, mamlaka zote, majina yote, usulutani wako wote na majeshi yako yote yameanguka (Isaya 21:9b)) kwa pigo la maji ya uzima yaliyotoka ubavuni mwa Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai.

         Kuanzia leo Yezebeli hauna mamlaka tena juu yangu, mji wangu, familia yangu, uzao wangu na wote wanaofungamana na maisha yangu, kazi zangu, na eneo lolote linalonihusu katika jina la yesu Kristo.Tena ninatangaza minyororo na kamba zote zilizokuwa zimenifunga, kamba za kifamilia,kiukoo,kikabila,kijamii na kitaifa kukatika na kuniachia mimi, mji wangu, familia yangu na uzao wangu kuanzia sasa kwa mamlaka ya jina la Yesu.

       Ninakiri na kutangaza ushindi juu yangu, familia yangu, mji wangu na uzao wangu tangu sasa katika jina la Yesu Kristo.Ninatangaza uzima juu yangu, waliokuwa hawajaolewa kuolewa na kuwa na ndoa bora yenye furaha, watoto wangu wa kiume/kike ambao walikuwa wamefungwa kuoa/kuolewa, sasa waoe/waolewe na kuwa na familia njema yenye ushindi, ustawi wa kiuchumi, afya bora katika miili yao, maendeleo katika kazi zetu za mashamba, mifugo, miradi, na kila tunachokifanya kifanyike Baraka katika jina la Yesu Kristo.


Wiki ya pili

     Hii itakuwa ni mfululizo wa siku nyingine saba za kupanda na kujenga Yeremia 1:9 – 10,Mwanzo 1:3-27).''Tazama nimekuweka juu ya falme na mamlaka ili kung'oa kubomoa na kuharibu kuangamiza ili kupanda na kujenga.'' wiki iliyopitailikuwa ni kung’oa kubomoa, kuharibu na kuangamiza.

Wiki hii ni ya kujenga, kumbuka Bwana Yesu alisema pepo amtokapo mtu, huenda akitafuta mahali pasipo na maji akikosa husema nitarudi katika nyumba niliyotoka. Tena hutafuta mapepo mengine Saba yaliyomabaya kuliko yeye na hali ya mtu Yule huwa mbaya kuliko ilivyokuwa mwanzo (luka11:24-26).Tunataka tukapande Roho saba za Mungu ndani na juu ya maisha yetu. Hizo Roho Saba za Mungu ndizo zitakazo chukua nafasi ya vile vichwa saba vilivyokuwa vikitawla juu nya maisha yetu vya yule mwanamke babeli.

                           Maombi yake yatakuwa ni haya:

Baba katika jina la Yesu ninakuja mbele zako umesema na tukikaribia kiti chako cha rehema kwa ujasiri. Nami sasa ninakikaribia kiti chako cha rehema nakuomba toba kwa ajili yangu mahali popote ambapo nimekutenda dhambi kwa kufahamu na pasipo kufahamu. Unirehemu sawa sawa na fadhila zako kiasi cha wingi wa rehema zako nakuomba ufute maovu, makosa, dhambi na machukizo yangu. Nioshe katika damu ya mwana kondoo Yesu Kristo, nitakase Bwana katika jina la Yesu nafsi yangu, Mwili na roho yangu.

Ninajipatanisha sasa na wewe kupitia damu yako katika jina la yesu Kristo. Ninasimama na damu yako katika ukuhani kwa ajili ya familia yangu, jamaa zangu, rafiki zangu, watoto wangu, mke/mume wangu, baba na mama yangu, wajomba na mashangazi, mama wakubwa/wadogo katika jina la yesu, ninaita utakaso wa damu ya yesu juu ya nafsi zao, roho na miili yao, maisha na kazi zao katika jina la Yesu.Ninawapatanisha na wewe kupitia msalaba/damu ya mwanao nafsi/roho na miili yao katika jina la Yesu Kristo.

Ninasimama kwa ajili ya jmaa,ukoo, kabila langu na taifa langu. Ni kweli yapo maovu yaliyotendeka kwa ngazi ya kikabila, Ukoo na taifa. Ninaleta maovu haya yote katika msalaba wako, ninakiri uovu wote mbele zako kama kuhani wako katika damu yako. Naomba usamehe na rehema zako uzielekeze kwetu. Tunajipatanisha na damu yako na kufanya amani na wewe Mungu wetu (efeso1:13-17), tunakukaribisha sasa uje na umiliki na kutawala juu yetu katika jina yesu Kristo “Ameni”

   siku ya kwanza

   Kupanda na kujenga mithali 9:1,mwanzo1:3-5

   Baba katika jina la Yesu wewe ndiwe uliyesema kwamba hekima ameijenga nyumba yake amesimamisha nguzo saba. katika jina la Yesu Kristo ninasimama sasa na agano hili la maji ya uzima kwa ajili ya kupanda na kujenga uzima juu na ndani ya maisha yangu.Ninapanda na kujenga yule Roho wa Bwana katika mji wangu, familia yangu, ndoa yangu, uzao wangu, ndani ya damu yangu, Mwilini mwangu, maishani mwangu, katika jina la Yesu Kristo, atawale na kumiliki.

Ninabatilisha uwepo wa Belzebel ndani yangu, juu yangu kwa watoto wangu, mke wangu, nyumba yetu, ukoo wangu kabila langu na taifa langu katika jina la yesu kiristo.Nafasi aliyokuwa belzebuli ninakusimamisha na kukupanda wewe Roho wa BWANA katika jina la Yesu. Ninaachilia maji ya uzima juu yako ee Roho wa Bwana yakuneemesha na kukustawisha ili uwe wa mizizi ndani yangu sawa na Yeremia 17:9 – 10.Amen.

Siku ya pili mwanzo 1:6-8  

   Ninapanda Roho wa hekima ya Mungu aliye hai maishani mwangu, ndani ya damu na mfumo wa maji mwilini mwangu, juu ya  mji wetu, familia, nyumba na uzao wangu, katika ukoo wangu, kabila langu na Taifa langu kwa mamlaka ya jina la Yesu, kupitia agano la maji ya uzima yaliyotoka ubavuni mwako, nabatilisha uwepo wa hekima ya kidunia na kipepo katika maisha yangu ndani yangu, damu na mfumo wa maji mwilini mwangu, familia yetu, mji wetu, ukoo wetu, kabila letu, jamaa zangu, Taifa letu na eneo lolote linalonihusu.Ninakiri uwepo wa hekima yako maishani mwangu, familia yangu, mji, ukoo, taifa na nyumba yangu.Ninaachilia maji haya ya uzima juu yangu, familia yangu, kabila, ukoo na taifa langu kwa ajili ya kustawisha na kuneemesha pando la Roho wa hekima ya Mungu alie hai, kama ulivyosema utaleta manyunyu kwa wakati wake, manyunyu ya Baraka (Ezekiel 34:26). Sasa yaachilie hayo maji ya ubavuni mwako kama manyunyu kustawisha na kuneemesha Roho huyU wa hekima katika maisha yangu,mji wangu,familia,ukoo,jamaa,kabila na taifa langu katika jina la Yesu kristo.

Siku ya tatu mwanzo 1:9-13

Ninapanda Roho wa ufahamu katika mji, ndoa yangu, kazi yangu, ukoo wangu, kabila langu, taifa langu, katika maisha yangu, ndani ya damu na mfumo wa maji mwilini mwangu.Ninabatilisha uwepo wa ufahamu wa kipepo unaotembea ndani na juu yetu tuliouridhi kwa mababa na mama zetu, familia tulizotoka, miji, ukoo, kabila na taifa kwa ujumla.Tunasimamisha na kupanda ufahamu wa Mungu aliye hai ndani na juu ya maisha yetu kupitia agano la maji ya uzima yaliyotoka ubavuni mwako na katika miji, familia,ukoo, kabila na taifa letu.Ninakiri uwepo wa ufahamu wako ee Yesu Kristo ndani na juu ya maisha yangu mji, famila, uzao, kabila, ukoo, Taifa langu lote.Ninatangaza ya kwamba Roho wa ufahamu wa Yesu Kristo tangu leo yuko ndani na juu ya maisha yangu, familia, mji, uzao wangu, kabila, ukoo na taifa akiachilia ufahamu wa Mungu kwetu unaotuongoza katika njia ya haki kweli.Katika jina la Yesu ninaona ufahamu wako Yesu Kristo ukibadilisha kabisa maisha na hatima ya maisha yangu, mji wangu, ukoo, kabila, uzao wangu na taifa.Ninaendelea kuachilia maji yako ya uhai juu yangu, mji wangu, familia, uzao wangu, kabila,ukoo na taifa langu yaendelea kuchilia mvua ya Baraka kwa ajili ya kustawisha ufahamu wako ee Yesu Kristo Bwana wangu siku zote na katika kila eneo la maisha Yetu.

   Siku ya nne:mwanzo 1:14-18

   Ninapanda Roho wa shauri katika maisha yangu, mji wangu, familia, ukoo, kabila, ndoa yangu, kazi, huduma na eneo lolote la maisha yetu.Wewe ndiwe uliyesema kwamba utanifundisha na kunionyesha njia utakayoiendea utanishauri jicho lako litanitazama (zab 32:8) sasa Bwana, katika jina la Yesu nahitaji huyo Roho wa ushauri apandwe ndani na juu ya maisha yetu ili kupitia Roho wako wa shauri atupe mashauri ya njia sahihi tutakayoiendea ili tusije tukapotea au kuenenda nje ya mapango wako.Kwa mamlaka ya jina la Yesu tunabatilisha uwepo wa yule Roho wa ushauri wa ibilisi aliyekuwa anatembea ndani na juu ya maisha yetu ambaye alikuwa anatupa mashauri yaliyo nje na makusudi yako ee Bwana Yesu.Ninakiri kuanzia sasa Roho wako wa ushauri atatuongoza katika shauri lako (zab 74:24), miji ,familia, kabila, koo na taifa letu kwa ujumla.Katika jina la Yesu Kristo kama vile mtumishi wako Daudi (2 Samweli 2:1) alivyokuwa akipata mashauri kwako katika mipango mbalimbali kwako, na jinsi ulivyokuwa ukimshauri katika njia ya mafanikio ndiyo na Roho wako wa shauri anavyotenda kazi ndani na juu ya maisha yetu kuanzia siku ya leo na hata milele  na milele .Amen.

    Siku ya tano mwanzo 1:20-23

   Ninapanda Roho wa uweza katika maisha yangu, mji wangu, familia, kabila, ukoo na taifa langu, kazi, ndoa na eneo lolote linalofungamana na maisha yangu katika jina la Yesu.

“Hili ndilo neno la Bwana kwa zerubabel, kusema sio kwa uwezo wala si kwa nguvu bali ni kwa Roho yangu asema Bwana wa majeshi (zacharia 4:6).Sawa sawa na neno lako ninamkiri huyo Roho wa uwezo ndani na juu ya maisha yangu, familia, mji, uzao, ndoa, mashamba, kazi, mifugo, uchumi wangu, kabila, ukoo, taifa, huduma yangu na eneo lolote la maisha yetu, ili aachilie uweza wake katika kutuwezesha kutenda mambo na kuyakamilisha.Kama Roho wa uweza alivyoonekana katika maisha ya Zerubabel ya kumpatia uwezo wa kujenga hekalu la Mungu, nasi tunamhitaji kwa ajili ya kuachilia uweza wake ndani yetu utakaotuwezesha kuwa watendaji katika jina la Yesu Kristo.Ninatangaza kubatilika kwa Roho wa uweza wa kipepo uliokuwa ukitembea ndani na juu ya maisha yetu kutoka kwa mababa na mama zangu upande wa baba na upande wa mama yangu.Kupitia agano hili la maji ya uzima yaliyotoka ubavuni mwako ninaona uweza wako ukidhihirika ndani na juu ya maisha yangu, familia yetu, mji wetu, uzao wangu, kabila langu, ukoo wangu, taifa langu, kazi yangu na eneo lolote linalohusu maisha yangu.Ninatangaza uwepo wa madhihiriko katika kila eneo la maisha yangu, mahuisho ya mji wangu, familia, uzao wangu, afya yangu mwili wangu, katika damu na mfumo wa maji yaliyoko ndani yangu, kazi zangu, uchumi wangu, ndoa yangu, maisha yangu katika jina la Yesu Kristo.Ninatangaza juu yangu na familia, mji, uzao wangu, uwezo wa kielimu, kiuchumi, kiroho, afya ya mwili na roho, maisha ya kila siku, kuoa na kuolewa kwa watoto wangu na kuwa na familia zao bora, kumiliki na kutawala katika ardhi.

 Siku ya sita mwanzo 1:24-31

  Ninapanda Roho wa maarifa katika maisha yangu, mji wangu, familia, kabila, ukoo na taifa langu, kazi, ndoa na eneo lolote linalofungamana na maisha yangu katika jina la Yesu.

Sawa sawa na neno lako katika mithali24:4''Na kwa maarifa vyumba vyake hujazwa'' ninamkiri huyo Roho wako wa maarifa ndani na juu ya maisha yangu, familia, mji, uzao, ndoa, mashamba, kazi, mifugo, uchumi wangu, kabila, ukoo, taifa, huduma yangu na eneo lolote la maisha yetu, ili aachilie ujazo wa kila jambo jema katika jina la yesu.Kama Roho wa Maarifa alivyomwezesha yesu  kristo kuwafanya wengi kuwa wenye haki nasi leo tunamhitaji katika jina la yesu kristo.Ninatangaza kubatilika kwa Roho wa maarifa ya  kipepo aliyekuwa akitembea ndani na juu ya maisha yetu kutoka kwa mababa na mama zangu upande wa baba na upande wa mama yangu.Kupitia agano hili la maji ya uzima yaliyotoka ubavuni mwako ninaona  maarifa yako yakidhihirika ndani na juu ya maisha yangu, familia yetu, mji wetu, uzao wangu, kabila langu, ukoo wangu, taifa langu, kazi yangu na eneo lolote linalohusu maisha yangu.Ninatangaza uwepo wa madhihiriko  ya maarifa ya Mungu katika kila eneo la maisha yangu, mahuisho ya mji wangu, familia, uzao wangu, afya yangu mwili wangu, katika damu na mfumo wa maji yaliyoko ndani yangu, kazi zangu, uchumi wangu, ndoa yangu, maisha yangu katika jina la Yesu Kristo.Ninatangaza juu yangu na familia, mji, uzao wangu, maarifa katika elimu,uchumi, kiroho, afya ya mwili na roho, maisha ya kila siku, kwa watoto wangu na  familia zao, maarifa yatuongezee uwezo (mithali24:5b) wa kumiliki na kutawala katika katika ardhi,kutunza familia zetu,fedha, kumiliki mashamba, kuwekeza, kutenda mambo yote mema ya kimaendeleo katika jina la Yesu Kristo.Tena umesema (Isaya 53:11a).Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki atawafanya wengi kuwa wenye haki'' nami ninatangaza maarifa yako katika mji wangu, nyumba,familia,ukoo,taifa,kabila  na jamaa zangu ili wote  yatuvushe katika maeneo mbalimbali ya maisha yetu.Amen

    Siku ya saba: mwanzo 2:1-4

  Ninapanda Roho wa kumcha Bwana katika maisha yangu, mji wangu, familia, kabila, ukoo na taifa langu, kazi, ndoa na eneo lolote linalofungamana na maisha yangu katika jina la Yesu.

''Kumcha  Bwana  ni chanzo cha maarifa''(mithali 1:7a).Sawa sawa na neno lako ninamkiri huyo Roho wa kumcha Bwana ndani na juu ya maisha yangu, familia, mji, uzao, ndoa, mashamba, kazi, mifugo, uchumi wangu, kabila, ukoo, taifa, huduma yangu na eneo lolote la maisha yetu, ili aachilie uweza roho wake kwetu katika kukutii wewe na kukuabudu.Ninatangaza kubatilika kwa Roho wa kumcha na kumtii shetani uliokuwa ukitembea ndani na juu ya maisha yetu kutoka kwa mababa na mama zangu upande wa baba na upande wa mama yangu.Kupitia agano hili la maji ya uzima yaliyotoka ubavuni mwako ninaona Roho wako wa kukucha akidhihirika ndani na juu ya maisha yangu, familia yetu, mji wetu, uzao wangu, kabila langu, ukoo wangu, taifa langu, kazi yangu na eneo lolote linalohusu maisha yangu.Ninatangaza madhihiriko ya kumcha Bwana  katika kila eneo la maisha yangu,mji wangu, familia, uzao wangu, afya yangu mwili wangu, katika damu na mfumo wa maji yaliyoko ndani yangu, kazi zangu, uchumi wangu, ndoa yangu, maisha yangu katika jina la Yesu Kristo.Ninatangaza juu yangu na familia, mji, uzao wangu uweza ule uliomwezesha Ibrahimu na Bwana yesu kristo kumtii Mungu  hadi mauti(wafilipi2:8). ...Tena alipoonekana  ana umbo kama mwanadamu ,alijinyenyekeza  akawa mtii  hata mauti,naam mauti ya msalaba.Bwana umesema basi nyenyekeeni chini ya mkono wako ulihodari ili utukweze kwa wakati wako,sasa ninaachulia Roho wako  wa  kumcha Bwana ili aendelee unyenyekevu  ndani na juu ya maisha yangu, familia, mji, uzao, ndoa, mashamba, kazi, mifugo, uchumi wangu, kabila, ukoo, taifa, huduma yangu na eneo lolote la maisha yetu.Ninatangaza utii wako katika mji wangu, nyumba,familia,ukoo,taifa,kabila  na jamaa zangu. .Ninatangaza juu yangu na familia, mji, uzao wangu, watu wote wamtii na kumwabudu Yesu kristo tena watetemeke mbele zake sawa na wafilipi2:9-10 katika jina la Yesu Kristo Amen.

 
KWA MAELEZO ZAIDI YA MAOMBI YA KUFUNGULIWA NA UKOMBOZI KATIKA

 FAMILIA WASILIANA NA MWALIMU KISANGA KWA SIMU NO.0719 949549

No comments:

Leave a Reply