Katika siku miamoja mnamo mwaka 1994, watu 800,000 waliuawa kinyama nchini Rwanda. Mauji hayo yalifanywa na wahutu wenye msimamo mkali.
Walikuwa wanawalenga watutsi waliokuwa wachache pamoja na wahutu wenye msimamo wa kadri.
Kwa nini wahutu waliwaua watutsi?Asilimia 85 ya wananchi wa Rwanda ni wa kabila la Hutu, lakini jamii ya
Tutsi imekuwa ikishikilia nyadhifa kubwa tu za ngazi za juu kwa miaka mingi.
Mwaka 1959, wahutu walimuondoa mamlakani mfalme wa Tutsi huku maelfu ya watu wa kabila hilo wakikimbilia nchi jirani kama vile Uganda.
Kikundi cha watutsi waliokuwa ukimbizini kikaunda vuguvugu waliloliita RPF ambalo lilivamia Rwanda mwaka 1990 huku vita vikiendelea hadi mwaka 1993 ambapo makubaliano ya amani yalifikiwa.
Lakini usiku wa terehe 6 Aprili mwaka1994, ndege iliyokuwa imewabeba hayati Rais Juvenal Habyarmana na mwenzake wa Burundi Cyprien Ntaryamira ilidunguliwa.
Kila mtu aliyekuwa katika ndege hiyo alifariki. RPF kilisema kuwa ndege hiyo iliangushwa na wahutu kama kisingizio cha mauaji kufanyika.
Waume waliwaua wake zao kwa hofu ya wao kuuawa
Mauaji ya Kimbari yalifanyika vipi?Kwa mpangilio wa hali ya juu. Orodha ya majina ya waliokuwa wanapinga serikali ilitolewa kwa wapiganaji ili waweze kuwaua pamoja na familia zao.
Majirani waliuana na hata waume wa kabila ta Hutu kuwaua wake zao wa Tutsi wakisema kuwa wangeuawa ikiwa wangetaa kufanya hivyo.
Wapiganaji walitumia vitambulisho vya watu kuwaua kwani majina yao yalionyesha ikiwa walikuwa wahutu au watutsi. Maelfu ya wanawake walifugwa kama watumwa wa ngono
Jumuiya ya kimataifa ililaumiwa pakubwa kwa kutizama tu mauaji yalipokuwa yanaendelea Rwanda
Nani alijaribu kusitisha vita?Umoja wa Mataifa na Ubelgiji zilikuwa na wanajeshi wao nchini Rwanda. Lakini umoja wa Mataifa haukuwa na idhini ya kusitisha mauaji.
Mwaka mmoja baada ya wanajeshi wa Marekani kuuawa Somalia, Marekani ilijitahidi kadri ya uwezo wake kujizuia kuingia katika vita barani Afrika.
Wanajeshi wa Ubelgiji walilazimika kuondoka nchini humo baada ya kumi kati yao kuuawa.
Walituhumiwa kwa kutofanya juhudi za kumaliza vita. Rais Paul Kagame ametuhumu Ufaransa kwa kuhusika na mauaji hao ingawa Ufaransa imekanusha vikali madai hayo.
Vita vilimalizika vipi?Chama cha RPF kikisaidiwa na Uganda , kilianza kudhibiti sehemu kadhaa za nchi hiyo hadi Julai tarehe 4, wanajeshi wake walipoingia mjini Kigali.
Wahutu milioni mbili wengi wakiwa raia walikimbilia nchi jirani ya DRC wakihofia kushambuliwa kama hatua ya kulipiza kisasi.
Watu milioni mbili wa kabila la Hutu walikimbilia nchi jirani kuepuka kisasi cha watutsi
Vipi hali ya Rwanda sasa?Rais Paul Kagame na chama chake RPF amesifiwa kwa kurejesha utulivu nchini Rwanda na hata kukuza uchumi wa nchi hiyo ndogo.
Pia amejaribu kuifanya Rwanda kuwa nchi inayong'aa kiteknolojia.
Lakini wakosoaji wake wanasema kuwa hapendi kukosolewa huku vifo vya wapinzani wake vikileta shaka.
Takriban watu milioni mbili walihukumiwa katika mahakama za jadi, viongozi wa mauaji wakihukumiwa katika mahakama maalum kuhusu mauaji ya Rwanda mjini Arusha Tanzania.
Kwa sasa ni hatia kwa mtu yeyote kuzungumzia ukabila nchini Rwanda, serikali inasema hii inasaidia kuzuia kutokea tena kwa mauaji kama hayo, lakini wakosoaji wa serikali wanasema hiki ni kiini macho tu kwani hisia zilizopo kuhusu ukabila huenda zikasababisha hali nyingine mbaya baadaye ikiwa watu hawatapewa uhuru wa kuzungumza.
(Source:BBC Swahili)
No comments: