Latest News


More

JE WAJUA JINSI YA KUKABILIANA NA UCHOVU?

Posted by : Unknown on : Wednesday, September 24, 2014 0 comments
Unknown
Saved under :

Jinsi ya Kukabiliana na Uchovu Mwingi

Anil, aliyekabiliana na uchovu mwingi
ANIL alikuwa amechoka kupita kiasi. Alikuwa amepata kazi mpya, nzuri, na yenye mshahara mnono. Lakini alilazimika kufanya kazi hadi usiku na wakati mwingine mwisho-juma, nyakati nyingine saa 80 kwa juma. Anasema: “Mazingira ya kazi yalikuwa magumu, na mimi ndiye niliyelaumiwa kwa sababu nilikuwa msimamizi. Nilijiuliza, ‘Nimekosea nini? Nisipofanya mabadiliko, nitakufa.’” Anil alikuwa amechoka kupita kiasi.
Uchovu unaotokana na kazi ni zaidi ya kuchoka kwa kawaida, na unazidi uchovu unaosababishwa na shughuli za kila siku. Dalili za uchovu huo ni kuchoka kupita kiasi kwa muda mrefu na vilevile kuhisi umekata tamaa na kukosa nguvu. Watu wanaokabili uchovu huo hawafurahii kufanya kazi zao, yaani, wanakosa hamu ya kufanya kazi na hivyo kuathiri ubora wa kazi. Utafiti pia unaonyesha kwamba kuchoka kupita kiasi husababisha matatizo ya kihisia na magonjwa.
Ni nini kinachosababisha uchovu mwingi? Kwa kawaida kazi nyingi kupita kiasi ndicho chanzo kikuu. Kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi, baadhi ya waajiri hutaka wafanyakazi wao wafanye kazi saa nyingi zaidi, na bila malipo ya kutosha. Maendeleo ya teknolojia hufanya iwe vigumu kwa watu fulani kutenganisha shughuli za kikazi na maisha ya binafsi. Nao wengine hupatwa na uchovu huo kwa sababu wanahofu kupoteza kazi zao, hawawezi kuzidhibiti, au wanahisi kwamba wanaonewa. Vilevile kutojua majukumu yao kazini au migogoro kati yao na wafanyakazi wenzao huchangia kuchoka kupita kiasi.
Uchovu mwingi pia unaweza kusababishwa na mtu mwenyewe. Ili wafikie malengo yao na kupata pesa nyingi, baadhi ya watu hufanya kazi zaidi ya moja. Watu hao wana majukumu mengi na wanakabili hatari ya kuchoka kupita kiasi.
Ikiwa unakabili tatizo la kuchoka kupita kiasi kazini, unawezaje kushinda tatizo hilo? Huenda ikaonekana vigumu kushinda tatizo hilo ikiwa kuna mambo yanayopita uwezo wako. Hata hivyo, chunguza hatua nne zifuatazo za kukabiliana na kuchoka kupita kiasi. Unaweza kupata suluhisho la tatizo lako.

 1. CHUNGUZA MAMBO UNAYOTANGULIZA.

Familia yenye furaha
Ni nini muhimu zaidi kwako? Watu wengi wanasema kwamba uhusiano na familia zao na afya njema ndiyo mambo muhimu zaidi. Hivyo, ukichoka kupita kiasi familia yako itaathirika na afya yako itazorota.
Ukizingatia mambo muhimu, itakuwa rahisi kwako kufanya maamuzi magumu na kukataa majukumu fulani. Kwa mfano, unaweza kugundua kwamba kazi yako inakusababishia uchovu unaopita kiasi. Hata hivyo, huenda ukasema, ‘Siwezi kubadili kazi au kupunguza muda ninaofanya kazi; ninahitaji pesa!’ Ni kweli, kila mtu anahitaji pesa, lakini kazi yako inaathirije mambo unayothamini zaidi?
Uwe mwangalifu ili usitangulize mambo ambayo wengine wanaona kuwa muhimu. Huenda mambo ambayo ni muhimu kwa mwajiri wako yakatofautiana na mambo yaliyo muhimu kwako. Wengine wanaweza kutanguliza kazi kuliko mambo mengine maishani, lakini haimaanishi unapaswa kufanya hivyo.
KANUNI YA BIBLIA: “HATA WAKATI MTU ANA VITU VINGI UZIMA WAKE HAUTOKANI NA VITU ALIVYO NAVYO.”—LUKA 12:15

2. RAHISISHA MAISHA YAKO.

mlo
Ili upunguze mkazo na upate muda wa kutimiza mambo unayothamini zaidi, huenda ukahitaji kufanya kazi kwa saa chache, kumwomba mwajiri wako akupunguzie majukumu, au ukahitaji kubadili kazi. Vyovyote vile, inaelekea utahitaji kupunguza matumizi ya fedha na kubadili mtindo wako wa maisha. Inawezekana kufanya marekebisho hayo, na huenda isiwe vigumu kama unavyowazia.
Katika nchi nyingi, wafanyabiashara wanashawishi watu wanunue bidhaa, na wengi wanafikiri kwamba furaha inatokana na kupata utajiri. Hata hivyo, si kweli. Maisha rahisi yanaweza kukuletea uhuru mwingi na kufanya uridhike. Ili ufanikiwe kufanya mabadiliko hayo, unahitaji kupunguza matumizi yako na kuweka akiba ya pesa. Jitahidi kupunguza au kuepuka madeni. Zungumza na familia yako kuhusu umuhimu wa mabadiliko hayo na uwaombe wakuunge mkono.
KANUNI YA BIBLIA: “TUKIWA NA CHAKULA NA KITU CHA KUJIFUNIKA, TUTARIDHIKA NA VITU HIVYO.”—1 TIMOTHEO 6:8

 3. JIFUNZE KUKATAA KAZI.

Ikiwa una kazi nyingi kupita kiasi au tatizo lenye kudumu kazini, zungumza na mwajiri wako. Ikiwezekana, toa mapendekezo yanayofaa hali yako na pia mwajiri wako. Mhakikishie mwajiri wako kwamba unapenda kazi, na ufafanue yale ambayo uko tayari kufanya; lakini utaje waziwazi na kwa uthabiti mambo ambayo huwezi kufanya.
Mwanamume anayetazama saa yake
Uwe mwenye busara na uone mambo kihalisi. Ikiwa unataka kufanya kazi kwa saa chache, huenda mwajiri wako akapunguza mshahara wako. Fikiria pia uwezekano wa kufutwa kazi, na uwe tayari kukabiliana na hali hiyo. Si lazima uache kazi ili utafute kazi nyingine, ni rahisi kupata kazi nyingine ukiwa bado kazini.
Hata kama mwajiri wako atakubali ufanye kazi kidogo ujue kwamba huenda baadaye akasisitiza ufanye kazi zaidi. Ni nini kitakachokusaidia kudumisha msimamo wako? Jitahidi kudumisha makubaliano yenu ya awali. Kufanya hivyo kutakupa uhuru wa kumwomba mwajiri aendelee kufuata makubaliano hayo.
KANUNI YA BIBLIA: “ACHENI TU NENO LENU NDIYO LIMAANISHE NDIYO, SIYOYENU, SIYO.”—MATHAYO 5:37

 4. UWE NA MUDA WA KUPUMZIKA.

Hata ukifaulu kupunguza kazi, huenda bado utapatwa na mkazo, utashughulika na watu wagumu, au hali zisizopendeza. Uwe na muda wa kupumzika vya kutosha na uwe na burudani kwa kiasi. Kumbuka kwamba si lazima utumie pesa nyingi ili ufurahie burudani pamoja na familia yako.
Mwanamke anapumzika huku akisoma
Mbali na kazi, uwe na mambo unayofurahia kufanya na pia uwe na marafiki, na uepuke kufikiria kazi tu kila wakati. Kwa nini? Kitabu Your Money or Your Life kinasema hivi: “Utu wako ni muhimu kuliko kazi unayofanya ili kupata pesa.” Ikiwa unafikiri utambulisho wako au heshima yako inategemea kazi yako, huenda ukashindwa kuweka mpaka kati ya kazi na shughuli zako mwenyewe.
KANUNI YA BIBLIA: “KONZI MOJA YA PUMZIKO NI AFADHALI KULIKO KONZI MBILI ZA KAZI NGUMU NA KUFUATILIA UPEPO.”—MHUBIRI 4:6
Je, unaweza kufanya mabadiliko ili ufanikiwe kukabiliana na kuchoka kupita kiasi? Bila shaka, unaweza. Anil, aliyetajwa mwanzoni mwa makala hii, alifanikiwa kufanya hivyo. Anasema hivi: “Niliwasiliana na mwajiri wangu wa zamani na kumwomba aniajiri tena, naye akakubali. Niliaibika kukutana tena na wafanyakazi wenzangu wa zamani kwa sababu nilikuwa nimewaambia kwamba nimepata kazi yenye mshahara mnono. Na nilipunguziwa mshahara. Lakini nilipata amani ya akili, na nikawa na muda zaidi wa kuwa na familia yangu na kufanya mambo muhimu.”

No comments:

Leave a Reply