Dar es Salaam.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema, amemsamehe Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye hivi karibuni alimtolea maneno makali kutokana na kutofautiana naye juu ya msimamo wa viongozi wa Kikristo kuhusu Katiba Inayopendekezwa.
Kardinali Pengo alitoa msamaha huo mbele ya waumini katika Kanisa la St
Joseph, Dar es Salaam jana, siku mbili baada ya Askofu Gwajima kuhojiwa na
Polisi kwa madai ya kumkashifu kiongozi huyo, mbele ya hadhara.
Askofu Gwajima anadaiwa kutoa kauli za kumkashifu kiongozi huyo kwamba
amewasaliti wa viongozi wenzake wa Kikristo kwa kuwataka waumini wa dini hiyo
kuamua wenyewe suala la Katiba Inayopendekezwa kinyume na msimamo wa waraka wa
kupinga katiba hiyo uliotolewa na Jukwaa la Wakristo Tanzania (CCT).
Baada ya kutolewa kwa waraka huo ulioagiza waumini kuipigia kura ya hapana
katiba hiyo, Askofu Pengo alinukuliwa akisema viongozi wa dini hawana mamlaka ya
kuzuia wananchi kuikubali Katiba hiyo huku akisisitiza waachiwe uhuru wao wa
kuamua.
Akizungumza jana wakati wa ibada ya Jumapili ya Matawi, inayoadhimishwa wiki
moja kabla ya Sikukuu ya Pasaka, Kardinali Pengo, bila ya kumtaja jina alisema:
“Natumia nafasi hii kueleza juu ya maneno ambayo yalitolewa na mchungaji fulani,
sikumbuki anaitwa nani… nasema nimemsamehe kutoka ndani ya moyo wangu wote,
anaweza kuwa na sababu zake ila nimemsamehe kabisa.
“Sina ghadhabu wala chuki ila kinyume chake, naomba tumwombee yeye na watu
wote waliokuwa wamehusika pengine nyuma yake ili Mungu aweze kutulinda na
kutudumisha katika hali ya amani ya Taifa letu.”
Alisema hatua ya Polisi kumkamata ni sehemu ya kutekeleza utaratibu wa jeshi
hilo tu, lakini yeye kwa nafsi yake ameshamsamehe.
Atolewa ICU, wafuasi wakamatwa
Katika hatua nyingine, Askofu Gwajima ametolewa kwenye chumba cha wagonjwa
wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) na kuhamishwa katika wodi ya kawaida baada
ya afya yake kuendelea vizuri.
Askofu huyo alikuwa ICU kwenye Hospitali ya TMJ, Mikocheni, alikofikishwa
usiku wa Ijumaa baada ya hali yake kubadilika ghafla alipokuwa akihojiwa Kituo
Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Askofu huyo alijisalimisha kituoni hapo akiitikia wito wa polisi uliomtaka
kufanya hivyo kutokana na tuhuma za kutoa lugha chafu dhidi ya Kardinali
Pengo.
Akizungumza jana, mke wa Askofu huyo, Grace Gwajima alisema baada ya
madaktari kumuona anaendelea vizuri, wameamua kumtoa ICU na kumpeleka kwenye
wodi ya kawaida.
(Source: Mwananchi Communication)
(Source: Mwananchi Communication)
No comments: