WAKATI mambo yakiwa bado tete juu ya afya ya kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la jijini Dar es Salaam, Mchungaji Josephat Gwajima, wafuasi wake wametangaza kufunga kwa muda wa siku 40 kuanzia juzi Jumatatu ili kuomba.
Chanzo kilicho ndani ya kanisa hilo ambalo kwa sasa makao makuu yake yapo Kawe, kililiambia gazeti hili kuwa wafuasi hao wameamua kuliacha suala hilo mikononi mwa Mungu, hivyo wameona ni vyema kufunga kwa muda huo ili kumuombea kiongozi wao apate afya njema, lakini pia misukosuko inayomuandama imalizike.
“Jamaa wameona hali sasa inakuwa ngumu, wanafunga kwa vikundi, kila mmoja anamuombea apate afya njema baada ya kuzidiwa wakati akihojiwa, lakini pia wanataka haya mambo yamalizike, kwa hiyo wameona ni bora kumuachia Mwenyezi Mungu ili ayamalize,” kilisema chanzo hicho.
Mmoja wa wachungaji viongozi wa kanisa hilo aliyeulizwa na gazeti hili juu ya jambo hilo, huku akitaka jina lake lihifadhiwe kwa vile siyo msemaji, alikiri waumini kuamua kufunga kwa vikundi, wakiomba katika maeneo yao ili afya na matatizo ya kiongozi wao yaishe haraka.
Mchungaji Gwajima alianguka ghafla wakati akihojiwa na maofisa wa Polisi wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, kufuatia maneno yake ya kashfa dhidi ya Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarb Kardinali Pengo.
Baada ya kuanguka, mchungaji huyo amekuwa akitibiwa katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni ambako hali yake imeelezwa kuwa bado tete, huku kukiwa na taarifa za kukamatwa kwa watu 15 wanaodaiwa kupanga mipango ya kumtorosha kiongozi huyo wa kiroho kutoka mikononi mwa polisi wanaomlinda.
(Source: Global Publisher)
No comments: