Johannesburg, Afrika Kusini. Jiulize, je, umeenda haja ndogo leo asubuhi au la?
Kama jibu ni ndiyo, basi ujue umemwaga kiasi
kikubwa cha nishati ambacho pengine kingeweza kuokoa kiasi cha fedha za
kulipia bili ya umeme nyumbani kwako. Pia, mkojo una manufaa zaidi
kwako ambayo huenda hukuyajua.
Wanayansi na watafiti nchini Uingereza wamevumbua
nguvu za mkojo katika kuzalisha nishati ambayo inaweza kuchaji simu kwa
muda wa dakika 25 na pia kumwezesha mteja kutuma ujumbe na kuperuzi
intaneti.
Watafiti hao kutoka Chuo Kikuu cha Watafiti cha
Bristol wakishirikiana na wenzao wa Maabara ya Robot wanasema kuwa
nishati hiyo ya mkojo ni mapinduzi ambayo yatasaidia katika upungufu wa
nishati wakati wowote badala ya kutegemea jua au upepo.
Timu ya watafiti hao iliweka mkojo katika chombo maalumu ambao baada ya muda ulizalisha bakteria.
Bakteria hao baada ya kuwa na njaa huzalisha
nguvu za kielektroni na kuwa nishati. Elektroni hizo hudondoshwa katika
kontena maalumu kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Mmoja wa wahandisi aliyevumbua nguvu za mkojo, Dk
Ioannis Ieropoulo wa Chuo Kikuu cha West of England (UWE), Bristol
anasema, mkojo ni bidhaa ambayo haiwezi kutupungukia tofauti na bidhaa
nyingine kama maji, upepo au jua.
Wavumbuzi hao wanasema mkojo ni nishati
inayopatikana wakati wowote hivyo hatua hiyo inasaidia kuwa na uhakika
wa kutopungukiwa na nishati hata kwa watu wa vijijini.
Anaongeza kuwa madhumuni hya uvumbuzi huo ni
kupata nishati inayopatikana wakati wowote, rahisi kuiunda na
itakayowasaidia watu wengi wa matabaka mbalimbali.
“Tumevumbua na tumehakikisha kuwa inafanya kazi.
Kilichobaki sasa ni kuangalia uwezekano wa mkojo kutumika katika
matumizi ya nyumbani,” anasema mhandisi huyo.
Mpaka sasa betri iliyoundwa kwa nishati ya mkojo
huo ina uwezo wa kuchaji simu itakayoweza kudumu kwa dakika 25, kutuma
ujumbe na kupiga simu kwa sekunde 20.
(Source: Mwananchi comm)
(Source: Mwananchi comm)
No comments: