Ndugu watano wafunga ndoa siku moja huko Kenya
Posted by :
Unknown
on :
Tuesday, August 6, 2013
0 comments
Nakuru.
Katika hali isiyo ya kawaida wanandugu watano kutoka familia moja wamefunga ndoa siku moja nchini Kenya.
Tukio hilo lililoibua mshangao miongoni mwa watu walioshuhudia lilitokea katika kanisa la mtakatifu Peter mjini Nakuru.
Maharusi waliojawa na furaha isiyo na kifani walielezea kuwa malezi yao bora yaliwafanya wote kuchagua kufunga ndoa siku moja.
Samson Wachira, ambaye ni wa kwanza kuzaliwa alisema wazazi wao waliwaonyesha kupendana na kushirikiana katika mambo yote tangu wakiwa wadogo hali iliyowapelekea kukua katika mazingira hayo.
Hivyo basi, Wachira alielezea kuwa kila mmoja wao alipotaka kufunga ndoa rasmi, aliwaita nduguze kwa ushauri.
Wachira ana mika 36 ilhali George Wango, ambaye ni wa mwisho kuzaliwa ana umri wa miaka 24.
Wengine walikuwa Peter Mbugua, 35, Stephen Kinyanjui, 34, na Harman Kago,32.
Ndugu hao waliitaja siku hiyo kama ya furaha ambayo walikuwa wakiingojea kwa hamu kubwa kutokana na kufikia kupiga hatua moja maishani mwao .
“Tumekuwa tukiingoja na kujitayarisha kwa siku hii kwa mwezi mmoja uliopita,” alisema Wango, mmoja wa maharusi hao
Wazo la kufunga ndoa siku moja liliwajia ndugu hao miezi saba iliyopita wakati kasisi mmoja alipowatembelea nyumbani kwao eneo la Kiratina.
Baba yao aliandaa karamu na ibada ya misa ya shukrani wakati kasisi alitaka kujua ni nani kwa familia hiyo alikuwa amekubaliwa kupokea sakramenti.
Kulingana na desturi za kanisa la Katoliki, ni sharti mwanamume awe amefunga ndoa rasmi kanisani ili kuruhusiwa kupokea sakramenti hivyo kasisi huyo aliwapa changamoto vijana hao kuhusu faida za kufunga ndoa kanisani.
Baada ya kushauriana baina yao, vijana hao walienda kuomba mawaidha kutoka kwa baba yao James Kago ambaye aliwapa moyo na kuwahamasisha kufunga ndoa siku moja.
“Niliwahimiza wafunge ndoa siku moja kwani hii ingewawezesha kufanya haraka, kupunguza gharama na zaidi ya hayo kuwaunganisha,” alisema Kago
Kwa mwezi mzima uliopita, familia ya Kago ilikua ikizunguka kwa wazazi wa wakwe zao watarajiwa mmoja baada ya mwingine ili kupeleka mahari na kuomba idhini ya kufunga ndoa rasmi.
Saved under :
Ndoa
No comments: