Latest News


More

SERIKALI YABANWA

Posted by : Unknown on : Monday, September 23, 2013 0 comments
Unknown
Saved under :
 
Askofu ataka ‘Big Results Now’ Sekta ya Afya ianze kwa nyongeza ya ruzuku
Na Suzanna Kipapy SERIKALI inapaswa kutoa ruzuku ya asilimia 100 kwenye mahitaji halisi ya huduma za afya katika Taasisi za Dini, kama inavyofanya kwa watumishi wa umma katika sekta hiyo. Hayo yameelezwa na Askofu Steven Mang’ana wa Kanisa la Mennonite alipokuwa akifunga Mkutano wa 76 wa mwaka wa Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa AMECEA, Kurasini Dar es Salaam. “Ili katika sekta ya afya tupate matokeo makubwa sasa ‘Big Results now’, tunaiomba serikali itoe ruzuku za afya kwa asilimia 100 ya mahitaji halisi na kwa wakati. Pia itoe marupurupu kwa watumishi wote kama inavyofanya kwa watumishi walioko kwenye sekta ya umma,” amesema Askofu Mang’ana. “Pamoja na hayo yote naishukuru Serikali kwa kupandisha hadhi Hospitali zetu kumi (10) ili kutoa huduma za Rufaa kwa ngazi ya Mkoa (Referral Hearth Services at Regional level) hii inaonesha jinsi Serikali inavyotambua na kuthamini huduma zitolewazo na vituo vyetu vya Kanisa.

Akizungumza na Wanachama wa TCMA, Askofu Mang’ana ambaye ni Mwenyekiti wa Maaskofu wa Kanisa la Menonite na Mwenyekiti wa Dayosisi ya Mashariki, amesema Wanachama hao kama Wakristo hawana budi kuwa mfano na Mawakili waaminifu wa Yesu Kristo, Katika utendaji wao kwa watu wanaowahudumia. Aidha amewaagiza Wanachama hao katika Umoja wao kujenga hospitali kubwa ya tiba na utafiti wa madawa na magonjwa mbalimbali yaani namna ya kuyagundua na kuyatibu ili iwe kama kumbukumbu yao kwa kutimiza miaka 76, kwa kuwa wanawajibika kuhakikisha watu wanapata tiba bora. Amekipongeza Chama Cha Madaktari Wakristo kwa juhudi zao wakishirikiana na Wamiliki wao kufikia mwaka 2012 kulikuwa na Hospitali Teule 37, hospitali za rufaa 13, vituo vya afya 107, zahanati 681 na kuridhika mchango mkubwa wa vituo hivyo vya Kikristo Tanzania.

 “Kwa kuangalia mahali Taasisi hizi zilipo na uwekezaji wake au thamani yake ilivyo kwa ujumla, ni dhahiri kwamba ni Mchango mkubwa ambao Wakristo wanatoa katika sekta ya afya kwa wananchi wa Tanzania, nimetaja hizo tu bila kutaja vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Makanisa. Anaongeza, “Kwa hakika unaona kuwa taasisi hizi zilijengwa na zitaendelea kujengwa katika maeneo ya pembezoni mwa nchi yetu ambayo mengi yalikuwa yamesahaulika katika mipango mikakati mbalimbali ya maendeleo nchini, na mmekuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM ya mwaka 2007 – 2017)” amesema Askofu Mang’ana. Katika hatua nyingine, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwa kuendelea kutambua na kuthamini mchango wa Kanisa nchini katika kuendeleza jamii kupata maisha bora na kutoa ruzuku ya uendeshaji huduma za afya.

 Baadhi ya Madaktari waliohudhuria Mkutano huo wameonesha kusikitishwa na serikali, kwani wakati mwingine watumishi wa afya wa umma hupata marupurupu kwa huduma ambazo bado wananchi wanawalalamikia kuwa ni hafifu na wakati taasisi wanazofanyia huwa zimefanya vizuri na wananchi wakipongeza kwa wazi huduma hizo. Akitoa tafakari, kabla ya kuanza Mkutano, Mchungaji Mallya wa KKKT Temeke amewahimiza Madaktari, mithali 23, “Linda sana moyo wako kuliko vyote ulindavyo” Amewataka pia kusikiliza dhamiri na daima kuwa na Moyo safi wa kumkaribisha Mungu na kuongozwa na Mungu daima katika utendaji wao na huduma yao kwa wagonjwa ili wao wenyewe wasijeruhiwe kidhamiri baada ya kuwatendea wagonjwa vibaya. Hamad Shaame ni Mfamasia wa Kampuni ya Salama Pharmaceuticals Ltd. iliyopo Jijini Dar es Salaam, ameshukuru chama cha Madaktari na Wauguzi Wakristo Tanzania kwa kuichagua Kampuni yao kuwa Mdhamini wa Mkutano wao wa mwaka. Akielezea historia ya Kampuni ya Salama Pharmaceuticals, amesema ilianzishwa mwaka 1986, wao ndiyo wasambazaji wakubwa wa dawa zilizothibitishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa kwa hapa Tanzania.
Ametaja malengo ya Kampuni hiyo kuwa ni kufikisha kwa wagonjwa bidhaa za afya zinazofuata utaalamu wa kiafya zinazowezesha ubora wa Maisha kwa wagonjwa na kuboresha matokeo na kufikisha bidhaa kupitia uongozi wa klinik, yenye matawi yake Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Moshi, Mbeya na itafungua matawi Dodoma na Morogoro. Mwenyekiti wa TCMA, Dk. Isaya Tosiri amesema katika risala yake kwa mgeni rasmi kuwa Mkutano huo wa 76, umejumuisha Madaktari, Wauguzi, Makatibu wa Afya na Wakuu wa Vyuo vya Afya vya Kikristo. Amesema huduma zitolewazo katika Hospitali, Vituo vya afya na Zahanati za Kikristo kwa nchi nzima ni zaidi ya asilimia 40, na vituo vingi vipo vijijini karibia kwa nchi nzima ambako miundombinu hairidhishi kiasi cha kutosha. Ameongeza, kwa upande wa serikali wameendelea kutoa ushirikiano kupitia mpango wake na sekta binafsi CPT, hata hivyo changamoto rasilimali watu yaani watendaji na wataalamu na changamoto ya kifedha na madawa zimebaki, hata kama daima wanajitahidi kutafuta suluhisho kuelezana mbinu mbalimbali za kimaendeleo ili kukuza kipato na kuongeza tija kwa wafanyakazi.

 Hata hivyo Dk. Tosiri, ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii kwa ushirikiano wanaouonesha katika kufanikisha utendaji wao. “ Pamoja na changamoto hizo tunashirikiana sana na serikali kupitia Wizara ya Afya katika kuendeleza huduma muhimu. Katika risala hiyo Dk. Tosiri amesema kila mwaka wanakuwa na maada maalumu ya kujadili katika kuhudumia wagonjwa, ambapo kwa mwaka huu wamejadili mambo muhimu/magonjwa matatu yanayowasonga Watanzania ambayo ni Hypertension (Ugonjwa wa shinikizo la damu), Diabetes (Ugonjwa wa Kisukari) na Asthma (Ugonjwa wa pumu), ambapo wamekaribisha Madaktari bingwa kuhusu magonjwa hayo.

Akitoa shukrani kwa Askofu kwa kufika kufungua Mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa TCSS, Bw. Peter Maduki amemshukuru Askofu Mang’ana kwa kufika kutekeleza wajibu wake. Bw. Maduki amemshukuru Askofu kwa hotuba yake, hasa alipowataka wanaTCMA, kutoa picha halisi ya huduma yao kama Wakristo, lakini amemtaka Askofu Mang’ana kwa niaba ya Maaskofu Wakristo wote na Viongozi wa dini Wakristo wanaomiliki huduma za afya kuwajibika. “Lakini Baba Askofu naomba nitoe maombi haya, kwa nini natoa maombi haya; Ni kwa sababu wewe na wenzio Maaskofu pamoja na viongozi wa dini wa Makanisa pamoja na CCT, na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, mnamiliki na mnashiriki kikamilifu katika utoaji wa huduma za Afya hapa nchini Tanzania. Ombi langu la kwanza; kumbukeni hivi sasa tunashirikiana na Serikali kwa kutumia sera ya Ubia, lakini katika utekelezaji wa sera ya ubia kumekuwa na changamoto zake, tunaomba wamiliki wa Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati, hasa Maaskofu na Viongozi wa Makanisa, mfahamu mwenendo wa utendaji kazi wa Serikali kwa kutumia ubia huu ili kushiriki kikamilifu katika kupambana na changamoto zilizopo” amesema Bw. Maduki

 Aidha kwa niaba ya Madaktari hao ameomba taratibu za uwezeshaji Hospitali zifahamike wazi, kwamba nani anateuliwa kuongoza na kusimamia hospitali, nani anawajibika kuhakikisha maslahi na haki za Wafanyakazi wanaotoa huduma katika kituo husika. Amewahimiza Maaskofu na Wamiliki wote wa huduma za kiafya zinazomilikiwa na Wakristo kuzidi kujenga uhusiano mzuri pamoja na kuwa na imani na Serikali kama wamiliki na siyo kuwaachia watendaji tu kujitahidi kujenga uhusiano huo. Mkurugenzi huyo mtendaji amezungumzia mikakati waliyopanga kuifanya Madaktari hao wa Kikristo kuwa baada ya miaka mitatu ijayo wataboresha huduma kwa asilimia 80, na kuhakikisha serikali na Makanisa wanatekeleza mikataba ya wafanyakazi ipasavyo. Katika kufanikisha huduma katika afya ya jamii wamepania kuongeza miradi ya kutosha ili kujenga uwezo kifedha, kusaidia upatikanaji wa dawa bora, zenye ubora na unafuu na kuifanya CSSC (Christian Social Services Commision) kuwa inayowajibika kwa kuwa na wataalamu. “Katika miaka mitatu ijayo tunatarajia kuona huduma za wagonjwa na wahudumu zinaboreshwa na kuona mahusiano mwema kati ya Serikali na Makanisa, hata hivyo tunafarijika kwani taasisi 867 za Kikristo zinatoa huduma hapa Tanzania kwa ubora na wengi wanavutiwa na huduma hizo”.

 Chama cha Madaktari Wakristo Tanzania, kilianzishwa Septemba 16, 1937 na kusajiliwa 1979, tangu kilipoanzishwa, kila mwaka wanachama wake hukutana na kuwekeana Mikakati mbalimbali katika kuhudumia Wagonjwa na kujadili masuala ya umoja wakizingatia pia sera ya Serikali katika masuala ya afya. Suzanna Kipapy OSB, ni Mtawa Mbenedictini wa Shirika la Mtakatifu Agnes, Convent ya Mtakatifu Getrude Imiliwaha- Jimbo la Njombe.

No comments:

Leave a Reply