WANAFUNZI
868,030 wanatarajiwa kufanya mtihani wakumaliza elimu ya msingi na maandalizi
yamekamilika.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, NaibuWaziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Bw.Philipo Mulugo, alisema mtihani huo unatarajiwa kuanza leo. Kati ya wanafunzi
wanaotarajiwa kufanya mtihani huo , wavulana ni 412,105 sawa na asilimia 47%,
wasichana ni 445,925 sawa na asilimia 52% .
Alitoa
wito kwa Maofisa Elimu katika mikoa na Halmashauri kuhakikisha taratibu zote za
mitihani zinazingatiwa pamoja na kuandaa mazingira salama yatakayozuia mianya
inayoweza kusababisha udanganyifu.“Nawaonya wasimamizi wote, wawe makini na
waadilifu katika kipindi chote cha mitihani, kujiepusha na vitendo vya udanganyifu
kwani Serikali haitasita kumchukulia hatua kali za kisheria mtu yeyote
atakayekiuka taratibu zilizopo,” alisema.
Aliwataka
wanafunzi wote kuzingatia taratibu za mitihani ili matokeo yao yaoneshe uwezo
wao halisi kulingana na maarifa waliyoyapata wakiwa shuleni kwa kujiepushe na
vitendo vya udanganyifu ili kuepuka kufutiwa mitihani yao. Alisema
wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao pembezoni mwa shule hizo, waondoke
katika maeneo hayo ili kuwapa nafasi nzuri wanafunzi kufanya mitihani yao kwa
utulivu zaidi.
Akizungumzia
mfumo wa usahihishaji Bw. Mulugo alisema umeonesha mafanikio makubwa katika
mitihani iliyopita kwani karatasi zote zilipita katika mashine maalumu bila
matatizo. Aliongeza kuwa, Serikali imetenga sh. milioni 400 kwa ajili ya
kuandaa vyeti ambavyo vinamfanya mwanafunzi atambulike kama mhitimu wa elimu ya
msingi.
“Fedha
hizi zimetengwa na Serikali, mzazi yeyote haruhusiwi kuchangia, kama yupo
ambaye atatozwa fedha atujulishe,” alisema. Awali, Bw. Mulugo alisema kati ya
malengo tisa ya mpango ya matokeo makubwa sasa (Big results now), kwa upande wa
sekta ya elimu Serikali ipo katika mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wa darasa
la pili watapewa mtihani ili kutambua uwezo wao wa kujua kusoma, kuandika kabla
ya kuendelea darasa tatu.
No comments: