Matukio ya
kumwagiwa tindikali yameendelea kukithiri huku Serikali ikiendelea kutoa ahadi
za kudhibiti bila mafanikio. Hivi karibuni baada ya raia wawili wa Uingereza
kumwagiwa tindikali Zanzibar, Serikali iliweka mikakati mikali ya kudhibiti
matumizi ya kemikali hiyo, lakini bado matukio hayo yameendelea kuwepo.
Tukio la
kumwagiwa tindikali kwa Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Cheju, Mkoa wa
Kusini Unguja, Joseph Mwang’amba ni mwendelezo wa uhalifu huo ambao Serikali
imeshindwa kabisa kuudhibiti.
Akieleza jinsi tukio hilo
lilivyotokea, Padri Mwang’amba anasema alikuwa nje ya duka linalotoa huduma za
mawasiliano ya mtandao (Sun Shine Internet Caffee) liliopo eneo la Mlandege
Wilaya ya Mjini Unguja, ndipo alipotokea kijana mmoja na kumwagia tindikali.
Wakati Padri
huyo akieleza hayo, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, ameijia juu polisi
kwa kushindwa kudhibiti matukio ya viongozi wa dini na Serikali visiwani humo,
kushambuliwa kwa kumwagiwa tindikali huku akilitaka kuwakamata waliohusika na
tukio hilo.
Kiongozi huyo wa
dini, aliyejeruhiwa maeneo ya usoni, mikononi na kifuani baada ya kumwagiwa
tindikali hiyo alisafirishwa jana na ndege ya kukodi ya Shirika la Coastal
kutoka visiwani humo hadi Dar es Salaam na baadaye kupelekwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Kwa upande wake,
Padri wa Parokia ya Mtakatifu Joseph, Zanzibar, Thomas Assenga aliyefuatana na
kiongozi huyo mpaka MNH, alisema siku za nyuma Padri Mwang’amba alitolewa
vitisho na mtu ambaye hamfahamu wakati akienda kutoa huduma katika kituo cha
wazee cha Welezo.
Alisema kabla ya kufika
kituoni hapo, kuna eneo ambalo nyakati za asubuhi watu hufanya mazoezi
barabarani ambapo kuna mtu mmoja alimtolea maneno ya vitisho.
Tukio hilo
linafuatia tukio la Agosti 7, mwaka huu ambapo raia wawili wa Uingereza, Kate
Gee (18) na Kirstie Trup (18) walimwagiwa tindikali katika maeneo ya Mji
Mkongwe, Zanzibar na vijana wawili waliokuwa wakiendesha pikipiki aina ya
Vespa.
Waingereza hao
walisafirishwa siku tatu baadaye kurudi kwao Uingereza kwa ajili ya matibabu.
Utetezi wa
Serikali
Siku tano baada
ya tukio la Waingereza hao kumwagiwa tindikali, Serikali kupitia vyombo vyake
vya uchunguzi iliwataka wananchi kuisaidia kuwafichua na kutoa ushahidi wa
uhalifu huo kwani ni vigumu kuwabaini wahusika.
Kauli hiyo ilitolewa kwa
pamoja jana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, Mkemia Mkuu wa
Serikali, Profesa Samwel Manyele na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP)
Eliezer Feleshi, katika mkutano wao na waandishi wa habari, uliolenga kueleza
mikakati ya kupambana na matumizi yasiyo sahihi ya tindikali nchini.
Picha na habari kwa hisani ya Mwananchi Communication!
No comments: