VYAKULA: Wengi hupenda nyama lakini wataalam wanatahadharisha
- Afya ya binadamu katika nyakati hizi imekuwa hatarini kuliko miaka ya nyuma kutokana na maradhi kuongezeka. Hivyo watu wameanza kula vyakula kwa kuchukua tahadhari na umakini mkubwa.
Mojawapo ni aina nyingi ya kemikali ambazo mtu anaweza kuzitia tumboni kwa
kivuli cha ‘chakula’ hivyo kuudhuru mwili.
Mwanataaluma wa Lishe, John Haule anasema chakula kinapoliwa na binadamu huwa
na safari ndefu na husafiri kwa zaidi ya saa 13 hadi 72 kulingana na kile
kilicholiwa.
“Utumbo mdogo au mwembamba una urefu mara nne ya urefu wa wastani wa mtu
mzima. Unakadiriwa kuwa na urefu wa futi 18 hadi 23. Isingekuwa kwamba
umesokotwa sokotwa kwa namna ya ajabu , usingeenea tumboni,” anasema.
Anafafanua kuwa tumbo limehifadhi vitu vingi na hivyo kuwa na uwezo wa kuweka
mipaka na kupangilia umeng’enywaji wa chakula kinacholiwa kila siku na hicho
ndicho hujenga na kuukarabati mwili wa binadamu.
“Tumbo la binadamu si kitu kidogo. Tumbo huweza kuhifadhi vyote unavyokula
kila siku huku vingine vikikaa tumboni kwa hata saa 72 bila kuyeyuka, kwa sababu
utumbo mwembamba tu wa binadamu una urefu wa futi 18 hadi 23 au mita saba ambazo
ni takriban sawa na urefu wa nguzo ya umeme wa nyumbani,” anabainisha.
Anasema utumbo huo umeungana na utumbo mnene. Huu una urefu wa futi tatu au
futi tano.
“Kwa hiyo ukipima urefu wa utumbo wote utastaajabu sana maana utapata futi 27
au mita nane na nusu,” anasema Haule.
Wakati wa umeng’enyaji, anasema tumbo hukutana na kibarua kigumu pale mtu
anapokula vyakula vinavyosindikwa viwandani ambavyo vina kemikali za kuvifanya
visiharibike mapema.
Anatoa mfano wa kemikali hiyo ya kuhifadhi vyakula husababisha ukinzani
wakati wa chakula kumeng’enywa tumboni na matokeo yake husababisha vitumie muda
mrefu ili kusanisiwa mwilini.
Vyakula vya namna hiyo, kama vile nyama nyekundu na vile vilivyopikwa na
mafuta mengi huweza kuchukua hadi saa 72, sawa na siku tatu kukamilisha kazi ya
umeng’enyaji.
Mazingira hayo ya chakula kudumu muda mrefu husababisha sumu kwenye vyakula
kuongezeka kama vile tindikali.
Anasema pia hujumuisha tindikali pamoja na vitu vingine hatari kwa afya kama
mafuta, lehemu, chumvi na kafeini ambavyo huathiri ini.
“Kwenye ini ndiko mifumo mingine huathirika na mtu kujikuta akiugua maradhi
ya moyo na damu kama vile shinikizo la damu, kisukari, kupooza na maradhi ya
mara kwa mara,” anasema.
Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma ya Ushauri Nasaha, Lishe na Afya, Mary Materu
anasema kutozingatia ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha ni chanzo cha kupata
magonjwa mengi yakiwamo saratani.
“Aina nyingi za saratani huanzia katika mtindo wa maisha na ulaji wa mhusika.
Mtu anapokula vyakula vinavyoushughulisha utumbo mwembamba na mpana kuchuja
vyakula hivyo kwa muda mrefu, husababisha maafa baadaye.
“Huanza kusababisha tumbo kujaa gesi, kuuma, kukosa haja na hata kukosa hamu
ya kula,” anasema.
Viko baadhi ya vyakula vinavyoweza kuongeza uwezekano wa kupata saratani.
Vyakula hivi mara nyingi ni vile vyenye mafuta mengi ambavyo vinasababisha uzito
mkubwa na huweza kumfanya mtu kupata magonjwa ya saratani ya matiti, kongosho na
kizazi,” anasema Materu.
Kuhusu nyama nyekundu yaani nyama ya mbuzi na ya ng’ombe, anasema ni moja ya
sababu zinazosababisha tatizo hilo.
“Nyama nyekundu ni muhimu sana kwa binadamu, lakini inapoliwa kupita kiasi
ni tatizo.Kwa kawaida binadamu anatakiwa kula nusu kilo ya nyama kwa wiki,
lakini walio wengi wanakula nusu kilo au zaidi kwa siku. Hilo ni tatizo,”
anasema huku akishauri watu wapendelee kula nyama nyeupe.
“Nyama nyeupe ambayo ni samaki, kuku na dagaa ni muhimu sana kwa mwili na
haina madhara sana kama ilivyo kwa nyama nyekundu ambayo ni ngumu katika
kumeng’enywa hivyo kutumia muda mrefu.”
Hata hivyo wataalamu walioangalia tafiti nyingi zilizofanyika kuhusu nyama
nyekundu na saratani, wameona upo uthibitisho wa kutosha kwamba ulaji wa nyama
nyekundu kwa kiasi kikubwa unaongeza uwezekano wa kupata saratani ya utumbo
mkubwa.
Tafiti huo umeonyesha kula hadi nusu kilo kwa wiki haiongezi uwezekano wa
kupata saratani, lakini kila gramu 50 inayoongezeka hufanya uwezekano wa kupata
saratani kwa asilimia 15.
Vyakula Vilivyosindikwa
(Source: Mwananchi communication)Vyakula Vilivyosindikwa
Haule amezitaja nyama zilizosindikwa pamoja na vyakula vingine vya aina hiyo,
hutumia muda mrefu kumeng’enywa.
“Vyakula vilivyosindikwa vimethibitishwa kwamba vinaongeza uwezekano wa
kupata saratani. Hata hivyo, wataalamu wanasema hawajaweza kuona kiasi chochote
cha nyama iliyosindikwa kinachoweza kutumika bila kuongeza uwezekano wa kupata
saratani,” anasema Haule. Nyama iliyosindikwa ni pamoja na ile iliyohifadhiwa
kwa kuongezwa chumvi, mafuta, kemikali au kukaushwa kwa moshi. Aina hii ya nyama
ni pamoja na nyama za kopo, soseji, bekoni na zinginezo.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Halifa Mkumbi anasema mtindo
wa maisha na ulaji ni kati ya vitu vinavyowaathiri wengi hasa katika nchi
zilizoendelea. Hata hivyo anasema mtindo wa maisha wa kutozingatia ulaji na
mpangilio wa vyakula ni kati ya vitu vinavyokuza magonjwa ya saratani ya tumbo,
utumbo na njia ya haja kubwa,” anasema.
Kukua kwa teknolojia pamoja na biashara, kumesababisha vyakula vya kusindikwa
kutumika hadi maeneo ya vijijini ambako siku za nyuma vilikuwa
havitumiki.
Kutokana na hali hiyo, magonjwa kama vile kisukari na maradhi ya moyo,
yaliwapata zaidi watu wa mijini lakini siku hizi yameenea hadi maeneo ya
vijijini.
Ili vyakula viweze kumeng’enywa vizuri, inashauriwa kula mbogamboga kwa wingi
pamoja na matunda.
Katika upikaji wa mboga, inashauriwa zisipikwe sana ili kutoharibu viinilishe
muhimu Ikiwezekana baadhi ya mboga ziliwe zikiwa mbichi ili kukamilisha lengo
hilo.
No comments: