Latest News


More

IBADA YA WANAUME YAFANA KANISA LA K.K.K.T USHARIKA WA MWENGE

Posted by : Unknown on : Sunday, June 8, 2014 0 comments
Unknown
 Leo katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (K.K.K.T) Usharika wa Mwenge imefanyika ibada nzuri ambayo imeratibuiwa na kuongozwa na wanaume wa Usharika huo
Katika ibada hiyo pia wanaume wa Usharika huo wameanzisha kwaya ambayo imeimba kwenye ibada hiyo ya leo
Pichani juu ni mratibu wa liturjia katika ibada hiyo mzee Godlisten Lema akiongoza ibada hiyo jumapili ya leo

Mwinjilisti Imbele akihubiri katika ibada ya wanaume jumapili ya leo ambapo alisisitiza wajibu wa wanaume katika kanisa na familia kwa ujumla
 Waumini mbalimbali wakiwa kwenye ibada hiyo ya wanaume wakiimba na kusifu
 Parish worker wa Usharika wa Mwenge Suzan Mwimbe (kushoto) akifurahia nyimbo za sifa
 Hakuna mzee wala kijana wote ilikua ni kucheza na kufurahi wakiwa nyumbani mwa bwana
 Mwalimu Kayesi (mwalimu wa kwaya za Usharika) akiongoza mapambio ya sifa jumapili ya leo
 Washarika wakiabudu na kusifu usharikani Mwenge leo

Ifuatayo ni risala iliyosomwa na Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya siku ya wanaume mzee Tumaini Kichila ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya mahusiano wa Usharika wa Mwenge

RISALA YA IBADA YA WANAUME LEO TAREHE 08/06/2014



1. UTANGULIZI

Wapendwa washarika wa Mwenge.Awali ya yote ninapenda kumshukuru sana Mungu wetu kwa niaba ya wanaume wote wa Usharika wetu kwa siku hii maalum na ya kipekee Ni siku ambayo wanaume wa usharika wetu tunafungua ukurasa mpya katika huduma katika kanisa letu la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (K.K.K.T), kwa kuanzisha umoja wa wanaume.

Wapendwa washarika, tunapenda kutoa Shukrani kwa uongozi wa Usharika kwa kuona umuhimu na kulipa jambo hili kipaumbele. Wazo la kuanzisha umoja wa wanaume tumekua nalo kwa muda mrefu na wakati ambao Mungu ametupa kibali ni hivi leo ambayo kwa mara ya kwanza tumekua na ibada ambayo inaratibiwa na wanaume.

2. MATARAJIO NA MALENGO

Ndugu washarika , ni matarajio yetu sisi kama wanaume wa usharika wa Mwenge kuwa Umoja huu hautaishia hapa tu siku ya leo bali ndio mwanzo wa huduma hapa Usharikani.Na ni ombi letu kwa uongozi wa Usharika ukiona vyema utupe kibali cha kutuweka kwenye ratiba ya kila mwaka kuwa na siku ya wanaume hapa Usharikani kwetu.

3. MALENGO

Malengo yetu ya awali katika kuanzisha umoja wetu huu kwanza ni kuimarisha nafasi yetu wanaume kwa kufanya kazi ya Bwana kwa uaminifu na uadilifu kwa kadri Mungu atakavyotupa kibali .

Ukisoma Yoshua 24: 1 “ Yoshua akawakusanya kabila zote za Israeli huko Shekemu, akawaita wazee wa Israeli, na wakuu wao, na waamuzi wao, na maakida wao, nao wakahudhuria mbele za Mungu.

Hivyo utaona ya kuwa wazee (wanaume) tuna nafasi muhimu sana kwenye familia na kanisa kwa ujumla
Pia ukisoma 1Timotheo 4:14 “Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na kwa kuwekewa mikono ya wazee”.

Nasi kama wanaume tuna karama Nyingi sana mbazo Mungu ametupa ambazo tunaweza kuzitumia kumtumikia Mungu wetu

Mkakati wetu wa kwanza tunauanza leo ambao ni wa kununua vyombo vya kisasa vya muziki vya usharika kwa ajili ya ibada.Vyombo hivi vitakua na thamani isiyopungua shilingi milioni 9 na ambavyo vitatumika kwa ajili ya ibada.Leo hii tunafanya uzinduzi wa sadaka hii.Mkakati huu unaanza na sadaka maalum itakayotolewa kwa njia ya bahasha maalum kwa washarika wote kama ilivyotangazwa , Lakini pia tutaendelea na kuhakikisha kwamba azma yetu hii inatimia.Hivyo tunaomba washarika wote mtuunge mkono katika mkakati wetu huu.

Mkakati wetu wa pili ni kudumisha na kuendeleza kwaya hii ya wanaume ambayo tunaamini itakua endelevu na ikiwezeka na hata kuhudumu mara moja kwa mwezi na kwa kuanza tutaona kwa pamoja namna tutakavyowezesha kutoa huduma kama kwaya yetu ya usharika wetu na hata mahali pengine japo mara moja kwa mwezi.
4. SHUKRANI
Shukrani za pekee ziwaendee kwanza kabisa ofisi ya Usharika wa Mwenge na baraza la wazee kwa kupanga mpango huu na kukubali kuanzisha umoja wa wanaume wa Usharika wetu.

Pili shukrani hizi ziwaendee wanaume wote wa Usharika wa Mwenge ambao nao kwa pamoja walilipokea wazo letu hili kwa mikono miwili ukizingatia ni wazo na kitu kipya si kwetu tu kama Usharika bali hata kwa Dayosisi ya Mashariki na Pwani kwa ujumla

Tatu kwa wanakamati binafsi ambao tumeshirikiana nao kwa namna moja au nyingine kufanikisha siku hii ya kipekee kwenye Usharika wetu hususan kwa wanakwaya ambao kwa muda mfupi tu wa takriban wiki mbili wameweza kuanzisha kwaya na kuweza kuimba siku hii ya leo, Mungu awabariki sana hakika kazi yenu si bure mbele za Bwana

Pia shukrani ziwaendee wanahabari wote ambao wamekubali kushiriki pamoja na sisi siku hii japo tuliwapa taarifa ya muda mfupi, tunasema Mungu na awabariki wote na kuwazidishia pale mlipotoa

5. MWISHO

Ni matumaini yetu kwamba huu utakua ni mwanzo mpya wa kazi ya Bwana kwa wanaume katika Usharika wetu huu wa Mwenge na tunatumaini washarika wote mtashirikiana nasi kuombea Umoja wetu huu ili uweze kusonga mbele siku zote


AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA NA MUNGU WANGU NA AWABARIKI
Tumaini Kichila
(Kwa niaba ya Kamati ya Mahusiano na

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya siku ya wanaume)

No comments:

Leave a Reply