AMKENI! JUNI 2014
KIKWAZO
Unapotazama orodha yako ya mapato na matumizi
unatambua kwamba pesa zinakuponyoka kama mchanga unavyopita katikati ya vidole.
Muda mrefu haujapita tangu ulipofunga ndoa, na unashindwa kudhibiti matumizi.
Je, utamlaumu mwenzi wako? Usikimbilie kufanya hivyo! Shirikiana naye kuchunguza
mambo ambayo huenda yamewaingiza nyote wawili katika hali hiyo. *
KISABABISHI NI NINI?
Mabadiliko. Kama ulikuwa
ukiishi nyumbani kabla ya kuolewa, huenda hukuzoea kulipa gharama za nyumbani na
kuchangia malipo. Inawezekana pia kwamba wewe na mwenzi wako mna maoni
yanayotofautiana kuhusu pesa. Kwa mfano, huenda mmoja wenu anapenda sana
kutumia pesa na yule mwingine anapenda kuweka akiba. Inachukua
muda kabla wenzi wa ndoa kufanya marekebisho na kukubaliana jinsi
watakavyopangia matumizi ya pesa.
Kuahirisha mambo. Jim, ambaye
sasa ni mwanabiashara mwenye mafanikio, anakiri kwamba mara tu baada ya kufunga
ndoa, alisumbuka sana kwa kushindwa kudhibiti matumizi. Anasema: “Kwa vile
nilichelewa kulipa gharama za nyumbani, mimi na mke wangu tulitumia pesa nyingi
kulipia gharama zilizochelewa. Tuliishiwa na pesa!”
Mtego “usioonekana wa pesa.”
Ni rahisi kutumia pesa kupita kiasi kama huoni zikitoka kwenye
kibeti chako. Huenda ikawa hivyo ikiwa unatumia kadi ya benki kulipia gharama
mbalimbali, au unanunua bidhaa kupitia Intaneti. Mtego wa kupata mkopo haraka
unaweza pia kuwanasa wenzi wapya wa ndoa.
Vyovyote vile, matumizi ya pesa yanaweza
kusababisha matatizo makubwa katika ndoa yako. “Watu wengi waliofunga ndoa
husema kwamba pesa ndilo tatizo kubwa, bila kuzingatia kiasi walicho nacho,”
kinasema kitabu Fighting for Your Marriage. “Pesa ndicho kisababishi
kikuu cha mizozano.”
UNACHOWEZA KUFANYA
Amueni kushirikiana. Badala
ya kulaumiana, shirikianeni kudhibiti matumizi yenu ya pesa. Anzeni kwa
kukubaliana kwamba hamtaruhusu matumizi ya pesa yawatenganishe.—Kanuni ya
Biblia: Waefeso 4:32.
Pangeni bajeti. Andikeni
gharama zenu zote kwa mwezi mmoja, kutia ndani gharama ndogondogo. Hilo
litawasaidia kujua matumizi yenu ya pesa na kutambua matumizi yasiyofaa. “Lazima
uache kumwaga pesa,” anasema Jim aliyetajwa mapema. “Yaani ujizuie kabisa.”
Andika orodha ya malipo muhimu, kutia
ndani chakula, nguo, kodi au malipo ya nyumba, gharama za gari, na mambo kama
hayo. Andika kiwango kinachohitajika kwenye kila sehemu, ili kuonyesha pesa
mtakazotumia katika kipindi fulani, labda kwa mwezi.—Kanuni ya Biblia:
Luka 14:28.
“Mkopaji ni mtumishi wa mtu
anayemkopesha.” —Methali 22:7
Tenga
pesa kila mwezi kwa ajili ya kila matumizi (chakula, kodi, mafuta ya gari, na
kadhalika). Watu fulani hufanya hivyo kwa kuweka pesa kwenye bahasha, kila
bahasha kwa matumizi hususa. * Pesa zikiisha
kwenye bahasha moja, wataacha kununua vitu vilivyotengewa bahasha hiyo au
kuchukua pesa kutoka kwenye bahasha nyingine.
Fikiria upya maoni yako kuhusu vitu
vya kimwili. Furaha haitegemei kuwa na vifaa vya kisasa. Yesu alisema:
“Hata wakati mtu ana vitu vingi uzima wake hautokani na vitu alivyo navyo.” (Luka 12:15) Kwa kawaida matumizi yako ya
pesa yanaonyesha kama unaamini maneno hayo.—Kanuni ya Biblia: 1 Timotheo 6:8.
Fanya marekebisho. “Ingawa
huenda mambo kama kuwa na televisheni ya kisasa na kula hotelini yakaonekana
yasiyogharimu mno, yanaweza kukuvuruga kifedha,” anasema Aaron, ambaye amekuwa
katika ndoa kwa miaka miwili. “Tulilazimika kujinyima mambo fulani ili tuishi
kulingana na mapato yetu.”
Maelezo ya Chini
^ fu. 4 Ingawa makala hii inawalenga wale ambao
wamefunga ndoa hivi karibuni, kanuni zinazotajwa zinawahusu wote waliofunga
ndoa.
^ fu. 14 Kama unalipia vitu kwa kutumia kadi ya
benki, weka orodha ya matumizi katika kila bahasha.
No comments: