Amri Zilizogawa Mabara
BAADA ya Christopher Columbus kurudi kutoka
safari yake ya kwanza kuizunguka Amerika katika 1493, wafalme wa Hispania na
Ureno walishindwa kukubaliana kuhusu ni nani atakayesimamia biashara na utawala
wa kikoloni wa maeneo hayo mapya yaliyogunduliwa. Hispania ilimwomba
papa, Aleksanda wa Sita, atatue mgogoro huo.
WAFALME NA MAPAPA WAGAWA MABARA
Hispania, Ureno, na Papa tayari walikuwa
wamefikiria kumiliki maeneo mapya yaliyogunduliwa. Katika mwaka wa 1455, Papa
Nicholas wa Tano aliipa Ureno haki zote za kuvumbua na kumiliki kila kitu
walichopata katika nchi na visiwa vilivyokuwa katika Pwani ya Bahari ya
Atlantiki katika Afrika. Kwenye Mkataba wa Alcáçovas wa mwaka wa 1479, Afonso wa
Tano wa Ureno na mwana wake, Prince John, walisalimu mamlaka yao juu ya Visiwa
vya Canary kwa Ferdinand na Isabella wa Hispania. Ikiwa sehemu ya makubaliano,
Hispania ilitambua mamlaka ya Ureno ya kufanya biashara katika Afrika na umiliki
wa Azores, Visiwa vya Cape Verde na Madeira. Miaka miwili baadaye, Papa Sixtus
wa Nne alithibitisha mkataba huo na kutaja kihususa kwamba ugunduzi wowote mpya
katika maeneo ya kusini na mashariki mwa Visiwa vya Canary, ungemilikiwa na
Ureno.
Hata hivyo, John, aliyekuwa John wa Pili wa
Ureno, alidai kwamba maeneo yaliyogunduliwa na Columbus yalimilikiwa na Ureno.
Watawala wa Hispania hawakukubaliana na uamuzi huo, hivyo wakakata rufaa kwa
papa mpya, Aleksanda wa Sita, ili awape haki ya kutawala na kuanzisha Ukristo
katika maeneo yaliyogunduliwa na Columbus.
Papa Aleksanda wa Sita aligawa mabara kupitia
maandishi tu
Ili kusuluhisha hilo, Aleksanda aliweka amri
tatu rasmi. Ya kwanza, “kwa mamlaka ya Mungu Mweza-Yote,” aliipa Hispania
pendeleo la pekee la umiliki usioisha wa maeneo mapya yaliyogunduliwa. Amri ya
pili iligawanya upande wa kaskazini hadi kusini uliokuwa na urefu wa kilomita
560, magharibi mwa Visiwa vya Cape Verde. Aleksanda alisema kwamba maeneo yoyote
yaliyokuwa tayari yamegunduliwa au ambayo yangegunduliwa upande wa magharibi wa
mstari huo, yangemilikiwa na Hispania. Papa aligawa mabara kupitia maandishi tu!
Amri yake ya tatu iliongezea Hispania umiliki katika upande wa mashariki wa
dunia hadi India. Hilo lilimkasirisha sana Mfalme John, ambaye watumishi wake
walikuwa wametoka tu kuzunguka kusini mwa Afrika, na hivyo kupanua mamlaka ya
Ureno kufikia Bahari ya Hindi.
RAMANI YAGAWANYWA TENA
Akiwa amechoshwa na Aleksanda, * John
alifanya makubaliano ya moja kwa moja na Ferdinand na Isabella. Mwandishi
William Bernstein anasema hivi: “Watawala wa Hispania walikazia fikira zaidi
kumiliki maeneo mapya katika Amerika na pia waliwaogopa sana Wareno waliokuwa
wakatili, hivyo walikuwa tayari kufikia makubaliano nao.” Hivyo, mnamo 1494
mkataba ulioitwa Tordesillas ulitiwa sahihi katika mji huo wa Hispania.
Mkataba wa Tordesillas ulidumisha mstari wa
upande wa kaskazini hadi kusini uliowekwa na Aleksanda, lakini ukauongeza mpaka
kufikia urefu wa kilomita 1,480 zaidi magharibi. Ilidaiwa kwamba bara la Afrika
na Asia “yalimilikiwa” na Ureno; na Amerika ilimilikiwa na Hispania. Kuhamishwa
huko kwa mstari mpaka upande wa magharibi, kulipanua eneo la utawala wa Ureno
mpaka kwenye eneo lililogunduliwa baadaye na kuitwa Brazili.
Amri zilizoipa mamlaka Hispania na Ureno
kumiliki na kutetea maeneo mapya waliyopata, zilitumiwa kama msingi wa umwagaji
mkubwa wa damu. Amri hizo zilipuuza haki za watu walioishi katika maeneo
yaliyogunduliwa kwa kuwakandamiza na kuwatendea isivyo haki. Zimekuwa pia chanzo
cha mgogoro wa karne nyingi miongoni mwa mataifa kuhusu umiliki na uhuru wa
kutumia bahari.
Maelezo ya Chini
^ fu. 9 Kwa habari zaidi kuhusu papa huyo
aliyejulikana kwa kuwa fisadi, tazama makala “Aleksanda wa Sita—Papa
Asiyesahauliwa na Roma,” katika gazeti la Mnara wa
Mlinzi, Juni 15, 2003, ukurasa 26-29.
No comments: