Jinsi ya Kushughulika na Mtoto Mwenye
Mtoto wako mwenye umri wa miaka miwili anapokasirika, anaanza kupiga kelele, anapiga-piga miguu chini kwa kishindo, na anajigaragaza chini. Unajiuliza: ‘Mtoto wangu yuko sawa kweli? Je, analipuka kwa hasira kwa sababu nimekosa kumtimizia mahitaji yake? Je, atawahi kuacha tabia hii?’
Unaweza kumsaidia mtoto wako mwenye umri wa miaka miwili abadili tabia yake. Lakini, kwanza, fikiria tabia hiyo inasababishwa na nini.
KWA NINI HILI HUTUKIA
Watoto
wadogo hawana uwezo wa kudhibiti hisia zao. Hali hiyo pekee inaweza kuwafanya
walipuke kwa hasira mara kwa mara. Hata hivyo, kuna sababu nyingine.
Fikiria
mabadiliko ambayo mtoto anapitia anapokuwa na umri wa miaka miwili hivi. Tangu
alipozaliwa, wazazi wake walimfanyia kila kitu. Kwa mfano, alipolia, wazazi
walikuja haraka. ‘Je, mtoto anaumwa? Je, ana njaa? Je, anahitaji
kubembelezwa au kubadilishwa nepi?’ Wazazi walifanya chochote
kilichohitajiwa ili kumtuliza mtoto wao. Ilikuwa sawa kufanya hivyo kwa sababu
mtoto anawategemea kabisa wazazi wake kwa kila kitu.
Hata
hivyo, anapofikia umri wa miaka miwili hivi, mtoto anaanza kutambua kwamba
wazazi wake hawafanyi tena mambo anayotaka wamfanyie. Kwa kweli, badala ya
wao kumtimizia matakwa yake, wanatazamia yeye atii
matakwa yao. Sasa mambo yamebadilika, na mtoto wa umri wa miaka miwili
hatakubali mabadiliko hayo kwa urahisi—huenda akalipuka kwa hasira.
Baada
ya muda, kwa kawaida mtoto anakubaliana na ukweli wa kwamba wazazi wake si
watunzaji wake tu bali pia ni wafundishaji wake. Inatumainiwa pia kwamba baadaye
atatambua kuwa jukumu lake ni ‘kuwatii wazazi wake.’ (Wakolosai 3:20) Kwa sasa, huenda mtoto
akawafanya wazazi washindwe kabisa kuvumilia milipuko yake ya
hasira.
MAMBO UNAYOWEZA KUFANYA
Elewa hali yake. Mtoto wako
si mtu mzima. Kwa kuwa hajui jinsi ya kushughulika na hisia zake, anaweza
kukasirika sana anapofadhaika. Jaribu kuona mambo kama yeye
anavyoyaona.—Kanuni ya Biblia: 1 Wakorintho 13:11.
Uwe mtulivu. Mtoto wako
anapolipuka kwa hasira, kukasirika hakutakusaidia. Kwa kadiri
inavyowezekana, puuza mlipuko wake wa hasira na udhibiti hisia zako. Kukumbuka
kwa nini milipuko ya hasira hutokea kutakusaidia kuwa
mtulivu.—Kanuni ya Biblia: Methali 19:11.
Shikilia msimamo wako. Ikiwa
unampa mtoto wako kila kitu anachotaka kwa sababu tu analipuka kwa hasira,
yaelekea ataendelea kufanya hivyo kila mara anapotaka kitu fulani. Kwa utulivu
mwonyeshe mtoto wako kwamba hutalegeza msimamo wako.—Kanuni ya Biblia:
Mathayo 5:37.
Kukumbuka kwa nini milipuko ya hasira hutokea kutakusaidia kuwa
mtulivu
Uwe na subira. Usitazamie
kwamba mtoto wako ataacha mara moja tabia ya kulipuka kwa hasira, hasa ikiwa
umempa sababu ya kuamini kwamba akilipuka kwa hasira utamruhusu afanye chochote
anachotaka. Hata hivyo, ikiwa unashughulikia hali kwa njia inayofaa na bila kuwa
kigeugeu, yaelekea milipuko ya hasira itapungua. Hatimaye, itaisha kabisa.
Biblia inasema: “Upendo ni wenye ustahimilivu.”—1 Wakorintho 13:4.
Pia
jaribu mambo yafuatayo:
-
Mlipuko wa hasira unapoanza mshikilie mtoto wako (ikiwa inawezekana) na, bila kumwumiza, mzuie asijigaragaze. Usimfokee mtoto wako. Subiri tu mpaka hali itulie. Hatimaye, mtoto atatambua kuwa kulipuka kwa hasira hakukumsaidia kwa njia yoyote.
-
Tenga mahali utakapomweka mtoto wako anapolipuka kwa hasira. Mwambie kwamba atatoka humo mara tu anapotulia, na kisha umwache humo.
-
Ikiwa mtoto wako analipuka kwa hasira mbele za watu, mwondoe hapo. Usimpe anachotaka eti kwa sababu tu amelipuka kwa hasira mbele za watu. Ukimpa, hilo linaweza kufanya afikiri kwamba ikiwa atalipuka kwa hasira, anaweza kupata chochote anachotaka.
No comments: