Kanisa la Anglikan Tanzania limepata askofu wake mpya leo baada ya aliyekuwa askofu wake Askofu Dr Valentino Mokiwa kustaafu rasmi leo.Askofu huyo mpya anaitwa Dr Jacob Chimeledya ambaye amesimikwa rasmi leo kuliongoza kanisa hilo.
Ibada hiyo imefanyika katika kanisa kuu la Roho Mtakatifu mjini Dodoma.Ibada hiyo iliyohudhuriwa na waumini wengi ilikuwa pia na viongozi mbalimbali wa serikali wakiongozwa na rais wa Tanzania Dr Jakaya Mrisho Kikwete.
Pichani juu Askofu mstaafu Dr Mokiwa akimsimika rasmi Askofu Dr Chimeledya kuongoza kanisa la Anglikan Tanzania
Askofu anayemaliza muda wake Dr Mokiwa akimtambulisha Rais Kikwete wa Tanzania askofu mkuu wa Cantebury askofu Justin Portal mara baada ya kumsimika askofu mkuu wa Anglikan leo
IFUATAYO NI HOTUBA YA RAIS KIKWETE KWENYE IBADA HIYO
Mhashamu
Justin Portal Welby, Askofu Mkuu wa Canterbury na Kiongozi wa Kanisa Anglikana
Duniani;
Mhashamu
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Jacob Erasto Chimeledya;
Wahashamu
Maaskofu Wakuu na Maaskofu wengine;
Mheshimiwa
Joseph Sinde Warioba na Mheshimiwa John Samweli Malecela, Makamu wa Rais na
Mawaziri Wakuu Wastaafu, Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Mawaziri, Wabunge,
Viongozi wa Ngazi Mbalimbali katika Serikali, Vyama vya Siasa na Jamii;
Viongozi
wa Dini na Waumini;
Wageni
Waalikwa;
Mabibi
na Mabwana;
Shukrani/Pongezi
Naomba
niungane na wenzangu walionitangulia kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa
Rehema, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa katika Kanisa Kuu la
Roho Mtakatifu Dodoma. Nawashukuru sana kwa heshima kubwa mliyonipa na
kunishirikisha kwenye tukio hili kubwa na la kihistoria kwa Kanisa la Anglikana
na nchi yetu. Najisikia kuwa mtu mwenye
bahati kubwa kuwa miongoni mwa waumini wa Kanisa la Anglikana kushuhudia
Mhashamu Askofu Erasto Chimeledya wa Dayosisi ya Mpwapwa akitawazwa kuwa Askofu
Mkuu wa Kanisa la Anglikana hapa nchini.
Karibu
Tanzania Kiongozi Baba Askofu Justin Portal Welby
Mkuu wa
Anglikana
Niruhusuni
niungane na wasemaji wenzangu walionitangulia kumkaribisha nchini kwetu Mhashamu
Justin Portal Welby, Askofu Mkuu wa Canterbury. Tunamkaribisha Tanzania na hasa
Dodoma kwa furaha na upendo mkubwa. Ameipa heshima kubwa nchi yetu, jambo ambalo
tutalienzi na kulikumbuka daima. Your Most Reverend, the Archbishop of Canterbury,
we warmly welcome you to Tanzania. Thank you for this big favour of coming in
person to grace this auspicious occasion. We deeply appreciate this gesture of
great love for the Anglican Communion and people of Tanzania. We will always be grateful and cherish this
moment.
Pongezi kwa
Baba Askofu Jacob Chimeledya Kutawazwa
kuwa Askofu
Mkuu
Mhashamu Baba Askofu Jacob Chimeledya;
Kwa
niaba yangu, ya Serikali na wananchi wa Tanzania nakupongeza sana kwa kuchaguliwa
kwako na leo kutawazwa kuwa Askofu Mkuu wa Sita wa Kanisa la Anglikana
Tanzania. Kuchaguliwa kwako kushika
nafasi hii kubwa kuliko zote katika uongozi wa Kanisa lako ni kielelezo cha
imani kubwa waliyonayo viongozi wenzake na waumini wa Kanisa la Anglikana hapa nchini.
Uwepo wa Baba Askofu Mkuu wa Canterbury, Mheshimiwa Justin Portal Welby, katika
hafla hii ni kielelezo kingine kikubwa cha kutambulika na kukubalika kwako na Kanisa la Anglikana duniani. Wote wanaamini
kwamba unao uwezo wa kuwaongoza vyema waumini wako katika mambo ya kiroho na
kimwili.
Napenda ujue kuwa
tunakupongeza kwa dhati, wakati huo huo tunatambua kwamba majukumu yaliyo mbele yako
si mepesi. Ni mazito na wakati mwingine yanaweza kuwa magumu pia. Kuna
changamoto nyingi ambazo bila shaka utakutana nazo. Tunakuombea kwa Mola
akuwezeshe kukabiliana na changamoto zote kwa mafanikio. Akujalie busara, subira,
uvumilivu, bidii na karama za uongozi ili uweze kumudu vyema majukumu yako mapya. Kwa sifa ulizonazo na uzoefu wa miaka mingi
katika utumishi wa Mungu na baraka zake nina imani kwamba utayamudu vizuri. Pamoja na hayo ni wajibu wa waumini wote na
kila mmoja wetu kuendelea kukuombea kwa
Mwenyezi Mungu ili akusaidie kumudu vyema majukumu mazito uliyokabidhiwa leo.
Mhashamu Askofu Mkuu Erasto
Chimeledya;
Kwa
upande wetu serikalini, napenda kukuhakikishia wewe, Maaskofu wenzako na
waumini wote wa Kanisa la Anglikana nchini kuwa tuko tayari kutoa kila aina ya ushirikiano utakaohitajika kwetu. Ushirikiano
tuliokuwa nao kwa muda mrefu tutauendeleza.
Niruhusu nitumie
nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Askofu Mkuu aliyekutangulia Baba Askofu
Valentino Mokiwa kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kipindi chake cha uongozi. Uhusiano kati ya Kanisa la Anglikana na Serikali
ulikuwa mzuri. Ninaamini chini ya uongozi wako, ushirikiano huo utaendelea kuimarika
na kufikia upeo wa juu zaidi.
Serikali
Inathamini Mchango wa Kanisha la Anglikana
Mhashamu Baba Askofu Mkuu;
Waheshimiwa Viongozi wa Dini;
Waumini na wananchi wenzangu;
Mimi
na wenzangu Serikalini tunatambua na kuthamini sana mchango mkubwa unaotolewa
na Kanisa la Anglikana kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Watanzania
wengi wamefaidi na wanaendelea kufaidika na huduma za elimu, afya, maji na nyinginezo zinazotolewa
na Kanisa la Anglikana. Kwa kufanya hivi Kanisa limekuwa likiunga mkono juhudi
za serikali za kuimarisha huduma za jamii na ustawi wa wananchi wake.
Nawapongeza na kuwashukuru
pia kwa juhudi zenu za kuwasaidia wananchi hasa vijana na wanawake wajenge
uwezo wao wa kuzalisha mali na kupunguza umaskini. Tafadhali endeleeni kuimarisha shughuli
mzifanyazo. Pia nimefarijika kusikia nia yenu ya kuanzisa Benki. Hii ni njia muafaka ya kuwawezesha watu kupata
mitaji nafuu na kwa urahisi. Nawaahidi ushirikiano wangu na wa Serikali yetu.
Ni kweli kuwa Serikali
kwa upande wake imekuwa inafanya yote haya. Wahenga wanasema “Kidole kimoja
hakivunji chawa”. Kwa Mashirika ya dini nayo yakichangia Watanzania wengi zaidi
wakiwemo waumini wenu watanufaika na maisha yao yatakuwa bora. Muumini
anayeishi kwenye lindi la umaskini ambaye hajui atapata wapi chakula au hajui atalala wapi na
kuvaa kwake ni kwa matatizo anaweza hata kukufuru kwa kuhoji huruma ya Muumba wake ipo wapi. Tukishirikiana
na tukisaidiana tutawapunguzia waumini majaribu hayo.
Viongozi
wa Dini Wahubiri Upendo na Mshikamano
Mhashamu Baba Askofu Mkuu Jacob
Chimeledya;
Nakubaliana
na wewe kuwa Watanzania tumekuwa tukiishi kwa amani na upendo bila kubaguana
kwa rangi, kabila, dini au mahali mtu atokapo.
Waasisi wa taifa letu - Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati
Mzee Abeid Amani Karume na viongozi wenzao na wale tuliofuatia tumetumia muda
mwingi kuhubiri amani, umoja, upendo na mshikamano. Dhamira yangu na viongozi wenzangu ni kuendeleza
na kudumisha tunu hizo na misingi hiyo mema ya taifa letu.
Inasikitisha
na kuumiza moyo kuona kuwa wapo baadhi ya watu hawapendi kuona nchi yetu ikiendelea
kuwa na amani, utulivu, umoja na mshikamano.
Hawapendi kuona Watanzania tukiishi kidugu na kushirikiana kwa pamoja
katika shida na raha, nyakati za sherehe na majonzi na masuala mbalimbali ya
jamii. Wanafanya kila mbinu ili
mfarakano utokee. Hivi sasa wanakazana kuchochea watu wabaguane, wachukiane na
hata wauane kwa misingi ya dini zao. Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na watu wenye mapenzi mema
na nchi yetu hatukubali wala hatutawaacha wafanikiwe katika dhamira zao za
kishetani.
Tumejizatiti ipasavyo
na tutaendelea kujiimarisha kwa kila hali kupambana na watu hao wasioitakia
mema nchi yetu. Kamwe hawatafanikiwa. Baadhi
yao wameshakamatwa na kufikishwa Mahakamani.
Kazi ya kuwatafuta washirika wao inaendelea na hatutachoka mpaka wote
wapatikane na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Ninachoweza
kuahidi ni kuwa serikali haitamuonea muhali mtu, watu au kikundi cha watu kinachochezea
amani ya nchi yetu na kuhatarisha usalama na maisha ya watu wake. Tutaendelea
kuwachukulia hatua. Kamwe hatuwezi
kuacha maisha ya watu wetu yapotee, amani ya nchi yetu ichezewe na mtu ye yote yule
kwa kisingizio chochote kile.
Naomba
viongozi wa dini muendelee kuliombea taifa. Pia muwaombee watu wenye nia mbaya
wageuke kuwa watu wazuri, kama Sauli
alivyogeuka kuwa Mtume Paulo. Endeleeni kuelimisha jamii na kuhubiri amani. Hakuna mwingine
anayeweza kuifanya kazi hiyo vizuri zaidi kushinda ninyi. Ninyi mnaheshimika sana kwa nafasi mliyonayo
katika jamii. Mafundisho yenu yanapokelewa kwa namna ya pekee na waumini
wenu. Tafadhali itumieni vizuri nafasi
hiyo adhimu kuhimiza moyo wa upendo, amani, umoja na mshikamano miongoni mwa
waumini wenu na Watanzania wote. Hubirini tuipende nchi yetu, tuwapende jirani
zetu na kila mtu ampende Mtanzania mwenzake.
Hubirini kwa uwezo wenu ili dhana ya upendo izame ndani ya mioyo yetu na
akili zetu. Tusaidiane kwenye shida na
raha. Tofauti za dini, rangi au kabila
zisitufarakanishe wala kutugawa. Tuishi
pamoja kwenye nchi yetu hii nzuri tuliyopewa na Mwenyezi Mungu.
Waheshimiwa Viongozi wa Dini;
Ndugu waumini;
Nayasema
kwa msisitizo maneno haya, kwa kutambua ukweli kwamba dini zote duniani
zinahimiza upendo miongoni mwa wanadamu bila kubagua. Zinawataka waumini wao kupendana
na kutendeana mema, na kuwapenda na kuwatendea mema waumini wa dini nyingine. Sio
kutendeana maovu. Dini zote duniani zinahubiri wanadamu kupendana, sio
kuchukiana, sio kuumizana na katu hakuna dini inayohubiri kuuana. Hivyo ndivyo
ilivyo kwa dini ya Kikristo, ndivyo ilivyo kwa Uislamu, ndivyo ilivyo kwa
Wahindu, Budha na kadhalika. Mtu hawezi kuwadhuru wafuasi wa dini tofauti na
yake eti kwa kisingizio cha kutekeleza matakwa ya dini yake. Mtu anayefanya
hivyo ana lake jambo. Hakuna dini inayowatuma wafuasi wake kufanya
maovu ya aina yoyote labda iwe dini ya Shetani.
Baba Askofu Mkuu;
Viongozi wa Dini;
Ndugu waumini na Wananchi;
Narudia
kuwaomba wanaofanya mihadhara ya dini, wahubiri dini zao bila ya kubeza au kukashifu dini za wengine. Mimi
siamini kuwa njia bora ya kumshawishi mtu akufuate ni kwa kumkashifu. Nadhani matokeo yanakuwa kinyume chake. Zingatieni
busara ya wahenga waliposema “maneno matamu humtoa nyoka pangoni”. Kwani lugha nzuri ya kushawishi haipo? Tafadhali
iondoleeni Serikali na vyombo vya dola ulazima wa kuwakamata na kuwafungulia mashtaka.
Mwisho
Mhashamu
Askofu Mkuu;
Wageni
Waalikwa;
Mabibi
na Mabwana;
Mwisho
narudia tena kuwashukuru viongozi wa Kanisa la Anglikana kwa kunialika kuja
kushiriki nanyi katika siku hii adhimu na ya kihistoria. Nalipongeza tena Kanisa Anglikana kwa mchango
mkubwa mnaoutoa kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Naomba tuendelee
kushirikiana kwani sote tuna kazi moja nayo ni kuwahudumia wanakondoo wa Bwana.
Mimi binafsi na Serikali ninayoiongoza nawaahidi ushirikiano usiokuwa na
masharti.
Baada
ya kusema hayo, narudia kutoa pongezi zangu za dhati kwako Baba Askofu Jacob
Erasto Chimeledya. Sote tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu akushike mkono na
kukuongoza katika kutekeleza majukumu yako. Nawaomba waumini wote mumpe ushirikiano
kiongozi wenu ili aweze kuifanya vema kazi aliyotumwa na Mwenyezi Mungu kufanya
kwenu, kwa Kanisa lake na nchi yake. Ninawatakieni nyote heri na fanaka tele
katika kusherehekea siku hii tukufu.
Asanteni.
Picha kwa hisani ya mitandao mbalimbali ya kijamii
No comments: