Askofu Malasusa: Tutashirikiana kupinga mauaji
Posted by :
Unknown
on :
Monday, November 25, 2013
0 comments
Ni ya kupinga mauaji ya vikongwe yanayoendelea kufanyika sehemu mbalimbali mkoani Shinyanga.
Shinyanga. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa amesema kanisa litahakikisha linashirikiana na Serikali katika kupambana na mauaji ya vikongwe hususani mkoani hapa ambapo wazee wamekuwa wakiuawa kila kukicha.
Hayo aliyasema jana wakati wa ibada ya sherehe ya kuwekwa wakfu kwa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria Usharika wa Ebenezer katika Kanisa Kuu mjini Shinyanga.
Askofu Malasusa alisema, Kanisa liko tayari kushirikiana na Serikali katika hili kwa madai kuwa mauaji hayo wakati mwingine yanasababishwa na wanadamu kukosa hofu ya Mungu na kutokuwa na elimu ya kutosha.
“Kwa kweli kanisa lina uwezo mkubwa wa kukomesha mauaji haya ambayo yanafanywa na watu wasiyo na upendo wa Mungu, kanisa lina mpango wa kupeleka injili hadi vijijini kunakofanyika mauaji hayo,”,alisema Malasusa na kuongeza: “Ndugu zangu mauaji haya yanalitia aibu kubwa taifa letu,sisi kanisa tunao wajibu wa kupiga vita mauaji haya kwani sheria sio kitu pekee cha kumbadilisha binadamu,”aliongeza Askofu Malasusa.
Awali akizungumza kanisani hapo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Annarose Nyamubi aliliomba kanisa kuisaidia Serikali mkoani hapa katika juhudi za kupiga vita mauaji ya vikongwe ambayo hivi sasa yanazidi kushika kasi hususani maeneo ya vijijini.
“Tunazishukuru taasisi za dini kwa kushiriki katika shughuli za maendeleo kama vile suala la elimu na afya, tunaomba pia mshiriki katika ulinzi na usalama kwani ndugu zetu wasiyo na hatia wanaangamia, jamani hakuna mwenye mamlaka ya kutoa uhai wa mtu bali ni Mungu pekee,” alisema mkuu wa wilaya huyo na kuongeza:
“Naleta kilio chetu mbele ya kanisa, kwani ndiyo mkombozi pekee aliyebaki. Hapa Shinyanga tumechoka kuendelea kusikia habari za mauaji ya vikongwe, naomba kanisa lifikishe injili vijijini,” aliongeza Nyamubi.
Saved under :
Habari za Kidini,
Neno la leo
No comments: