MKE WA WAZIRI MKUU Mama Tunu Pinda amewaeleza wanandoa kuwa ndoa ndiyo taasisi ya kwanza kuwafundisha watu maadili na kumjua Mungu pasipo Mungu haiwezekani.
Amesema hayo wakati
akifungua rasmi semina ya wanandoa wa kuanzia siku moja hadi miaka 25
iliyoandaliwa na watoa huduma wa New Life in Christ (Maisha Mapya Ndani ya
Kristo) siku ya jumamosi mchana tarehe 29 Machi, 2014 katika Ukumbi wa Msimbazi Centre
jijini Dar es salaam.
“Ndoa ndiyo Taasisi ya
msingi na ya kwanza kabisa kati ya Taasisi zote katika jamii ya mwanadamu ambayo
ilianzishwa na mwenyezi Mungu”, alisema Mama Pinda.
Taasisi hii ni muhimu sana
kwani ndiyo chanzo cha Familia na ndio chanzo cha jamii ya watu na mataifa
mbalimbali hivyo wanandoa wote inawapasa kuwa wa kwanza katika kukuza maadili
kwa kufuata maandiko ya mwenyezi mungu.
Mama Tunu Pinda alisema,
katika Kitabu cha Mwanzo, sura ya kwanza aya ya 27-28 inasema kwamba mungu
aliwaumba mtu mume na mtu mke kisha akawabariki akisema: “Zaeni na mkaongezeke,
mkaijaze Dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani na
kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi”
“Wanandoa hamnabudi
kujenga maadili mazuri,masikilizano na uvumilivu katika ndoa ili muweze kuepusha
uvunjifu wa maadili katika ndoa”. Inaaminiwa kwamba matatizo mengi ya kuporomoka
kwa maadili katika ndoa chanzo chake kikubwa ni kukosekana kwa uvumilivu,
alifafanua Mama Pinda.
“Ndoa zisipokuwa imara
watoto wanakosa malezi, ndoa zinapovunjika, si wanadoa tu wanaoharibikiwa, bali
watoto pia hupata majeraha makubwa ya kisaikolojia katika maisha yao,hivyo
nawaomba wanandoa kuisha katika imani na masikilizano ili kuweza kudumisha ndoa
zenu”, alisisitiza.
Semina hii ni chachu na
sehemu muhimu sana ya kujifunza na kukumbushana masuala muhimu ya kujenga ndoa
zenu, hivyo mtumie nafasi hii kutafakari hali halisi ya ndoa zenu kwa kuwa
wasikivu na wachangiaji wa mawazo na pia kwenda kuwaeleza na wengine kile
mlichojifunza: “Naamini semina hii italeta uponyaji na nuru mpya katika ndoa
zenu na familia na kuwa kichocheo katika kuimarisha ndoa zenu”,
alisema.
Napenda kusisitiza kwamba,
hatuwezi kuwa na Taifa la watu wenye maadili mema kama ndoa zenu ambazo ni kiini
cha familia, jamii na Taifa hazitaimarishwa, ni dhahiri kwamba hatutaweza kupata
viongozi bora ikiwa ndoa zilizo imara ambazo ni kiini cha uhai wa familia
zitaachwa ziyumbe:” Viongozi bora hutoka kwenye ndoa bora ni vizuri kujenga
utamaduni katika jamii kwa kuwa na ndoa zisizotetereka”alisema Mama
Tunu.
Mama Pinda aliwaomba watoa
huduma wa "New Life in Christ" pamoja na makanisa na watu wengine wanaotoa
huduma za mafundisho ya uimarishaji wa ndoa kufanye jambo hili kuwa endelevu na
kuhusisha ndoa nyingi kadri iwezekanavyo. “Serikalini wanasema Matokeo ya
Haraka sasa au Big Results Now nami nashauri iwe hivo katika ndoa zenu yawe
malengo yenu na yaelekezwe katika kuleta Matokeo Makubwa Zaidi”, aliongezea Mama
Tunu Pinda.
Mama Pinda aliwashauri
watoa huduma wa "New Life in Christ", kuangalia namna ya kuandaa Semina kwa
ajili ya vijana ambao sasa wameingia katika ulimwengu wa utandawazi kwa
kuwaaandaa na kuwasaidia waingie kwenye taasisi ya ndoa kwa kumshirikisha Mungu
kupata wenza wao kuliko kutafuta wachumba kupitia mitandao ya kijamii kama vile
facebook, viber, Instagram na mingineyo. “Semina hizi zitawasaidia kuwajenga
kimaadili huku wakitambua majukumu yao kama mume ama mke, kama baba au mama na
hatimaye kuishi katika maadili mema”.
Mapema, Mwenyekiti wa "New Life in Christ" Dkt. Alyson
Mmanyi alisema huduma kama hizi za semina zinatolewa kwa watu wote wakristo wa
madhehebu mbalimbali ili kuweza kunusuru ndoa na uvunjifu wa maadili kwani
Taasisi ya ndoa imevamiwa na ndoa bila Mungu
haiwezekani.
”Tumekuwa tunatoa huduma za
kuhubiri Injili kwa watu mbalimbali ambapo tayari tumeshatoa huduma hizi Mkoani
Tarime, Rorya na tunatarajia kwenda Butiama mwaka huu”,alisema Dkt.
Alyson.
(mwisho)
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
S. L.
P. 3021,
DAR ES
SALAAM.
JUMAMOSI, MACHI,28
2014.
No comments: