Dar es Salaam. Kuna kila dalili kwamba mwimbaji maarufu wa
muziki wa Injili nchini, Flora Mbasha na mumewe Emmanuel Mbasha wanatamani
kurudiana, baada ya kuwapo mgogoro katika uhusiano wao wa ndoa, ulioingia katika
vyombo vya habari yapata mwezi mmoja sasa.
Kwa nyakati tofauti jana, kila mmoja wao alimwambia mwandishi wetu kwamba
yupo tayari kurudiana na mwenzake, hatua ambayo inaweza kuondoa mgogoro huo
ambao umefifisha taswira yao ya kiutumishi.
Akizungumza nyumbani kwake Tabata Kimanga, Dar es Salaam, Mbasha alisema
ameshamsamehe mkewe na kwamba anamsubiri muda wowote arudi nyumbani kusuluhisha
mgogoro wao.
“Nawapenda Watanzania wote wazidi kutuombea ili mimi na mke wangu
turudiane.”
Kauli hiyo ni sawa na ile aliyoitoa Flora wiki iliyopita pale aliposema:
“Ninawaomba Watanzania waendelee kuniombea ili niweze kushinda majaribu haya,
kilichotokea ni sehemu tu ya kupimwa imani yangu”.
Jana, Flora alirudia kauli hiyo kupitia kwa wakili wake, Addo Mwasongwe
ambaye alisema mwimbaji huyo yupo tayari kukutana na mumewe na ndugu ili waondoe
tofauti zao.
Maelezo ya Mbasha
Kwa upande wake Mbasha alisema: “Mi namwomba Flora ajishushe akubali, aje
home (nyumbani) tuyamalize na maisha yaendelee. Yeye ni mke wangu namtaka. Kama
ananipenda arudi, tuite wazazi tutatue mgogoro huu.”
Aliongeza kuwa hakuna binadamu yeyote asiyesamehewa na kwamba kilichotokea
katika ndoa yao ni sehemu ya maisha ambayo wengi hupitia.
“Siku zote naamini tunachotakiwa ni kujenga na siyo kubomoa… Flora
asing’ang’anie kwa watu arudi hapa… apige hodi… ‘mume wangu’ nimerudi …na mimi
nitampokea tuendelee kulea watoto.”
Mbasha anakabiliwa na tuhuma za kumbaka shemejiye wa miaka 17 na kesi yake
inaendelea katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala na sasa yupo nje kwa
dhamana.
Kauli ya Flora
Wakili Mwasongwe alisema: “Flora amesema ameshayatoa rohoni masuala yote ya
mgogoro na mumewe na leo (jana) aliniambia anataka kusuluhishwa hata kesho (leo)
lakini nimeshindwa kuwakutanisha kwa sababu nipo ‘busy’.
“Ila nilimwambia Ijumaa hii nitafanya hivyo kwa kuwakutanisha yeye (Flora),
Mbasha na wazazi wake ili kumaliza tofauti hizo.”
Wakili huyo alisema awali alikutana na wazazi wa Mbasha lakini hawakufikia
mwafaka, lakini kwa sasa anaamini mambo yatakwenda vizuri
(Source:Mwananchi Communication)
(Source:Mwananchi Communication)
No comments: