Latest News


More

by : Unknown

Mkuu wa wilaya ya Kinondoni mheshimiwa Paul Makonda jumapili hii alikua mgeni rasmi katika uzinduzi wa vitabu vya injili vya mwalimu Lilian Ndegi katika kanisa la Living Water Center - Makuti Kawe

Bwana Makonda (pichani juu) alimshukuru mwalimu Lilian Ndegi jinsi Mungu anavyomtumia kuponya roho za watu kwa njia ya vitabu na alisema yuko tayari kushirikiana naye kuhakikisha vitabu hivyo vinawafikia watu wengi zaidi
 Pichani juu Bwana Makonda akikata utepe kuashiria uzinduzi wav itabu hivyo



Wakina mama wa kanisa waliandaa  keki maalum  kwa ajili ya mwalimu Lilian Ndegi

Bwana Makonda akimshukuru Tumaini Kichila kwa ununuzi wavitabu vya mwalimu Lilian Ndegi

 Mgeni rasm bwana Paul Makonda kushoto  akiwa na mtume Apostle Ndegi (mkuu wa kanisa la Living Water Center - Kawe) na mwalimu Lilian Ndegi ambaye ndiye mwandishi wa vitabu hivyo
 Wakina mama wa Kawe wakiunga mkono katika uzinduzi huo wa jumapili


 Badhi ya vitabu mbalimbali  (pichani juu na chini) ambavyo vimetungwa na mwalimu Lilian Ndegi




Wamama wa Kanisa la Living Water Center Waliandaa keki maalum kwa Mwalimu Lilian Ndegi
Mwalimu Lilian Ndegi akimlisha mumewe Apostle Ndegi Keki
Mwalimu Lilian Ndegi akimlisha mgeni rasmi bwana Paul Makonda keki



Posted on : Tuesday, July 21, 2015 [0] comments Label:

WAKRISTO WA LEO, JE TUNAHITAJI KUFUATA AMRI ZA AGANO LA KALE?

by : Unknown
Jambo muhimu la kufahamu ni kwamba agano la kale lilipatiwa taifa la Israeli wala sio wakristo. Baadhi ya sheria hizo zilikuwa za kuwafanya waisraeli wajue jinsi ya kumtii na kumfurahisha Mungu (amri kumi za Mungu kwa mfano), baadhi yazo zilikuwa zikiwafunza jinsi ya kumuabudu Mungu (kwa ile njia ya sadaka), nyengine zilikuwa za kuwafanya waisraeli wawe watu maalum (kama sheria za aina za mavazi na chakula). Hakuna sheria yoyote ya agano la kale inayotumika kwetu sasa. Yesu alipokufa msalabani, alimaliza matumizi ya sheria ya agano la kale (Warumi 10:4; Wagalatia 3:23-25; Waefeso 2:15).

Mahali pa sheria ya agano la kale, tuko chini ya sheria ya kristo (Wagalatia 6:2) ambayo ni, “Mpende bwana Mungu wako na moyo wako wote akili zako zote na nguvu zako zote. Hii ndiyo ya kwanza na amri iliyo kuu. na ya pili ni kama ya kwanza, mpende jirani yako kama nafsi yako. Torati yote na manabii inakamilishwa katika amri hizi mbili” (Mathayo 22:37 – 40). Tukifanya mambo haya mawili tutakuwa tunatimiza yale kristo angetaka tuyafanye, “na huu ndio upendo wa Mungu: kutii amri zake. Na amri zake si nzito” (waraka wa kwanza wa Yohana 5:3). Kwa mtazamo, amri kumi za Mungu hazina uhusiano na wakristo. Hata hivyo, tisa katika amri kumi za Mungu zimerudiwa katika agano jipya (zote isipokuwa ile ya kuweka sabato). Kwa kwaida kama tunampenda Mungu hatutakuwa na miungu miginemila yeye. Tukiwapenda majirani zetu hatutawaua, hatutawadanganya,hatutazini nao, wala kutamani kile walichonacho. Kwa hivyo hatuko chini ya sheria ya agano la kale. Sisi ni wakumpenda Mungu na pia majirani zetu. Tukifanya mambo haya mawili kwa uaminifu wa moyo, kila kitu kitakuwa sawa.
Posted on : [0] comments Label: ,

JEWEWE UNATOA FUNGU LA KUMI?

by : Unknown
Kutoa fungu la kumi ni jambo ambalo wakristo wengi hung’ang’ana nalo. Katika makanisa mengine kutoa fungu la kumi imesisitizwa kupita kiasi. Wakristo wengi pia hukataa kutii agizo la kutoa sadaka kwa Bwana. Kutoa fungu la kumi au sadaka inahitajika kuwa ni kitendo cha furaha na baraka. Lakini sivyo katika makanisa ya sasa.

Kutoa fungu la kumi ni agizo la agano la kale. Hili lilikuwa sharti la kila mwenye kupata zao au mfugo alete sehemu ya kumi ya pato hekaluni (mambo ya walawi 27:30; hesabu 18:26; kumbukumbu la torati 14;24; mambo ya nyakati ya pili 31:5). Wengine huchukulia ya kuwa fungu la kumi, katika agano la kale ilikuwa kama sehemu ya ushuru uliokuwa ukitolewa kwa ajili ya makuhani na walawi. Agano jipya haiamrishi wala kupendekeza mfumo halali wa kutolea fungu la kumi. Paulo asisitiza kuwa waumini watenge sehemu ya mapato yao kwa ajili ya kusimamia kanisa (wakorintho wa kwanza 16:1-2).

Agano jipya halielezi kiasi cha pato ambacho ni kitengwe kwa ajili ya kusimamia kanisa. (wakorintho wa kwanza 16:2). Kanisa la kikristo leo limechukua kile kiwango cha fungu la kumi kutoka kwa agano la kale na kukisisitiza kuwa ndicho kiwango cha chini cha mkristo kutoa. ijapokuwa agano jipya haitoi kiwango cha kutoa, inaelezea umuhimu na manufaa ya kutoa. Ni watoe sawa na uwezo wao “ kulengana na pato lake.” Wakati mwingine ina maana ya kutoa zaidi ya fungu la kumi, na mara nyingine kichache kuliko fungu la kumi. Yote hutegemea uwezo wa mkristo mwenyewe na mahitaji ya kanisa. Kila mkristo sharti aombe na kutafuta hekima kutoka kwa Mungu juu ya swala hili (Yakobo 1:5). “ kila mtu niatoe kile alicho azimia kutoa kutoka ndani ya moyo wake, si kwa manung’uniko wala kulazimishwa, kwa kuwa Mungu hupenda kwenye kutoa kwa moyo mkunjufu” (wakorintho wa pili 9:7).
Posted on : Thursday, April 23, 2015 [0] comments Label:

WAJUA KWA NINI MUNGU ALIKUUMBA?

by : Unknown

Jibu la Biblia

Mapenzi ya Mungu ni kwamba umjue Yeye vizuri, umkaribie, na kisha umpende na kumtumikia kwa moyo wako wote. (Mathayo 22:37, 38; Yakobo 4:8) Unaweza kujifunza jinsi ya kufanya mapenzi ya Mungu kwa kuchunguza maisha na mafundisho ya Yesu. (Yohana 7:16, 17) Yesu hakuongea tu kuhusu mapenzi ya Mungu—aliishi kupatana na mapenzi hayo. Kwa kweli, Yesu alisema kwamba kusudi kuu maishani mwake ni ‘kufanya, si mapenzi yake, bali mapenzi ya aliyemtuma.’—Yohana 6:38.

Je, ninahitaji ishara, maono, au mwito wa pekee ili nijue Mungu aliniumba kwa kusudi gani?

Hapana, kwa sababu Biblia ina ujumbe wa Mungu kwa wanadamu. Ina kila kitu unachohitaji ili ‘uwe na vifaa kamili kwa ajili ya kila kazi njema.’ (2 Timotheo 3:16, 17) Mungu anataka utumie Biblia pamoja na ‘nguvu zako za kufikiri’ ili ujifunze mapenzi yake.—Waroma 12:1, 2; Waefeso 5:17.

Je, kweli ninaweza kufanya mapenzi ya Mungu?

Ndiyo, unaweza, kwa kuwa Biblia inasema hivi: “Amri za Mungu si ngumu sana kwetu.” (1 Yohana 5:3, Easy-to-Read Version) Hilo halimaanishi kwamba ni rahisi kufuata amri za Mungu kila siku. Lakini, faida unazopata ni nyingi sana zinapolinganishwa na jitihada zako. Yesu mwenyewe alisema hivi: “Wenye furaha ni wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika!”—Luka 11:28.


Posted on : [0] comments Label:

BIBLIA INARUHUSU KUJICHANJA CHALE?

by : Unknown

Jibu la Biblia

Biblia inataja kuhusu kuchanja chale mara moja tu katika kitabu cha Mambo ya Walawi 19:28, ambapo tunasoma hivi: “Msijitie alama ya chanjo.” Mungu aliwapa Waisraeli amri hiyo, na hivyo kuwafanya tofauti na watu waliowazunguka ambao walijitia alama za majina au maumbo ya miungu yao mwilini. (Kumbukumbu la Torati 14:2) Ingawa Sheria ambayo Mungu aliwapa Waisraeli haiwahusu Wakristo, tunapaswa kuzingatia kanuni inayotegemea sheria hiyo.

Je, Mkristo anapaswa kuchanja chale au kuuchora mwili wake?

Maandiko yafuatayo yanaweza kukusaidia ujue jinsi ya kutenda:
  • “Wajipambe kwa mavazi yenye . . . kiasi.”—1 Timotheo 2:9 New World Translation) Kanuni hiyo inawahusu wanaume na wanawake. Tunapaswa kuheshimu hisia za wengine na kuepuka kujifikiria wenyewe.
  • Wengine wanataka watambuliwe na watu au waonekane wako huru, ilhali wengine wanajichanja chale ili waonyeshe kwamba wanajiamini. Hata hivyo, Biblia inawatia moyo Wakristo ‘watoe miili yao kuwa dhabihu iliyo hai, takatifu, yenye kukubalika kwa Mungu, utumishi mtakatifu pamoja na nguvu zao za kufikiri.’ (Waroma 12:1) Tumia ‘nguvu zako za kufikiri’ kuamua ni kwa nini unataka kujichanja chale. Ikiwa unafanya hivyo kwa sababu unataka kufuata mtindo fulani au kuonyesha kwamba wewe ni mshiriki wa kikundi fulani, kumbuka kwamba kujichanja chale kuna madhara ya kudumu. Kuchunguza nia yako kunaweza kukusaidia kufanya uamuzi wa hekima.—Methali 4:7.
  • “Mipango ya mwenye bidii bila shaka huleta faida, lakini kila mtu anayetenda haraka-haraka bila shaka huuelekea uhitaji.” (Methali 21:5) Mara nyingi uamuzi wa kujichanja chale hufanywa bila kufikiria kwa uzito, na unaweza kuathiri uhusiano wako na wengine au kazi. Ni ghali sana kuchanja chale na kuna maumivu mengi sana unapoamua kuziondoa. Utafiti—kutia ndani biashara iliyositawi ya kuondoa watu chale—inaonyesha kwamba idadi kubwa ya watu waliojichanja chale wanajuta ni kwa nini walifanya hivyo.
by : Unknown


Jibu La Biblia

Katika Biblia, mara nyingi namba hutumiwa kwa kihalisi, hata hivyo nyakati nyingine hutumiwa kwa njia ya mfano. Muktadha wa andiko unaweza kutusaidia kujua ikiwa namba fulani inatumiwa kwa njia ya mfano au la. Fikiria baadhi ya namba ambazo zinatumiwa kwa njia ya mfano katika Biblia:
  • 1 Umoja au muungano. Kwa mfano, Yesu alimwomba Mungu kwamba wafuasi wake “wote wapate kuwa kitu kimoja, kama vile ambavyo wewe, Baba, umo katika muungano pamoja na mimi na mimi nimo katika muungano pamoja na wewe.”—Yohana 17:21; Mathayo 19:6.
  • 2 Katika mambo ya kisheria, mashahidi wawili huthibitisha ukweli wa jambo fulani. (Kumbukumbu la Torati 17:6) Vivyo hivyo, kurudia maono au maneno fulani kulihakikisha kwamba jambo hilo lilikuwa hakika na la kweli. Kwa mfano, Yosefu alipokuwa akifasiri ndoto ya Farao wa Misri, alisema hivi: “Kwa kuwa ndoto hiyo ilirudiwa mara mbili kwa Farao inamaanisha kwamba jambo hilo limewekwa imara na Mungu wa kweli.” (Mwanzo 41:32) Katika unabii, “pembe mbili” zinaweza kuwakilisha serikali pacha, kama vile nabii Danieli alivyoambiwa kuhusu Milki ya Umedi na Uajemi.—Danieli 8:20, 21; Ufunuo 13:11.
  • 3 Sawa na vile mashahidi watatu wanavyoweza kuhakikisha kabisa jambo fulani kuwa la kweli, kurudia jambo mara tatu kunakazia au kuonyesha kwamba linalosemwa ni hakika.—Ezekieli 21:27; Matendo 10:9-16; Ufunuo 4:8; 8:13.
  • 4 Namba hii inaweza kumaanisha ukamili katika umbo au katika utendaji, kama vile katika maneno “pembe nne za dunia.”—Ufunuo 7:1; Isaya 11:12; Ufunuo 21:16.
  • 6 Kwa kuwa namba hii imepungua saba inayowakilisha ukamilifu, sita inasimamia kutokamilika au lisilo kamilifu, au jambo linalohusianishwa na maadui wa Mungu.—1 Mambo ya Nyakati 20:6; Danieli 3:1; Ufunuo 13:18.
  • 7 Namba hii hutumiwa mara nyingi kumaanisha ukamilifu. Kwa mfano, Waisraeli waliagizwa na Mungu kuzunguka jiji la Yeriko kwa siku saba, na kuizunguka mara saba katika siku ya mwisho. (Yoshua 6:15) Biblia ina mifano mingi ambapo namba saba imetumiwa kwa njia hiyohiyo. (Mambo ya Walawi 4:6; 25:8; 26:18; Zaburi 119:164; Ufunuo 1:20; 13:1; 17:10) Yesu alipomwambia Petro kwamba amsamehe ndugu yake “si, Mpaka mara 7, bali, Mpaka mara 77,” kurudia namba 7 kulionyesha kwamba alipaswa kuendelea kusamehe “bila kuacha”.—Mathayo 18:21, 22.
  • 10 Namba hii inaweza kuwakilisha jumla ya kitu, au kukusanya pamoja.—Kutoka 34:28; Luka 19:13; Ufunuo 2:10.
  • 12 Namba hii inaweza kumaanisha ukamili kuhusiana na kusudi la Mungu. Kwa mfano, mtume Yohana alipewa maono ya kimbingu ambapo aliona jiji lililokuwa na “mawe ya msingi kumi na mawili, na juu ya hayo majina kumi na mawili ya mitume.” (Ufunuo 21:14; Mwanzo 49:28) Namba 12 ikizidishwa mara kadhaa pia inaweza kuwa na maana hiyohiyo.—Ufunuo 4:4; 7:4-8.
  • 40 Baadhi ya hukumu au adhabu ilihusianishwa na namba 40.—Mwanzo 7:4; Ezekieli 29:11, 12.

Ubashiri kwa kutumia namba

Jinsi ambavyo namba imetumiwa kwa njia ya mfano katika Biblia ni tofauti na jinsi inavyotumiwa katika kubashiri. Watu wengine hufanya uchawi kwa kutumia namba, kupatanisha namba, na kujumlisha namba mbalimbali ili kubashiri matukio. Kwa mfano, kikundi fulani cha Wayahudi kimechunguza maana zilizofichika kwenye Maandiko ya Kiebrania kwa kutumia njia inayoitwa gematria, ambayo inahusisha kutafuta namba fulani ya siri katika namba zinazolingana kwenye herufi. Ubashiri wa kutumia namba ni namna ya uaguzi, tendo ambalo Mungu anakataza.—Kumbukumbu la Torati 18:10-12.
Posted on : [0] comments Label:

SAYANSI INAPATANA NA BIBLIA?

by : Unknown


Ndiyo, hata ingawa Biblia si kitabu cha kisayansi, inazungumzia mambo ya kisayansi kwa usahihi. Fikiria mifano fulani inayoonyesha kwamba sayansi inapatana na Biblia na kwamba Biblia yenyewe inataja mambo hakika ya kisayansi yanayotofautiana na yale ambayo watu walioishi zamani waliamini.
  • Ulimwengu ulikuwa na mwanzo. (Mwanzo 1:1) Tofauti na hilo, hekaya nyingi za kale zinasema kwamba ulimwengu haukuumbwa, ulijitokeza wenyewe. Wababiloni waliamini kwamba miungu iliyozaa ulimwengu ilitoka katika bahari mbili. Hekaya nyingine zinasema kwamba ulimwengu ulitoka katika yai kubwa sana.
  • Ulimwengu unaongozwa na sheria za asili, si utendaji wa miungu. (Ayubu 38:33; Yeremia 33:25) Hekaya mbalimbali ulimwenguni pote zinafundisha kwamba wanadamu hawawezi kufanya jambo lolote isipokuwa kile kilichoamuliwa na miungu inayotenda mambo yasiyotarajiwa na yenye ukatili.
  • Dunia inaelea angani. (Ayubu 26:7) Watu wengi walioishi nyakati za kale waliamini kwamba dunia ni tambarare na kwamba imeshikiliwa na jitu fulani au mnyama, kama vile nyati au kasa.
  • Maji yanayoingia katika mito na vijito huwa yamevukizwa kutoka baharini au kutoka katika vyanzo vingine kisha yanamwagika tena yakiwa mvua, theluji, au mvua ya mawe. (Ayubu 36:27, 28; Mhubiri 1:7; Isaya 55:10; Amosi 9:6) Wagiriki wa kale walifikiri kwamba maji ya mito yalitoka kwenye bahari iliyo chini ya ardhi, na wazo hilo liliendelezwa hadi karne ya 18.
  • Milima huibuka na kuporomoka, na wakati fulani milima iliyopo leo ilikuwa chini ya bahari. (Zaburi 104:6, 8) Tofauti na maoni hayo, hekaya fulani zinasema kwamba milima iko jinsi ilivyo leo kwa sababu iliumbwa na miungu.
  • Mazoea mazuri ya kutunza usafi hulinda afya. Sheria ambayo Waisraeli walipewa, ilitia ndani maagizo ya kwamba mtu anapaswa kuoga baada ya kugusa maiti, watu waliokuwa na magonjwa ya kuambukiza walipaswa kutengwa, na kinyesi kilipaswa kuzikwa. (Mambo ya Walawi 11:28; 13:1-5; Kumbukumbu la Torati 23:13) Tofauti na hilo, wakati ambapo sheria hizo zilikuwa zikitolewa, Wamisri walikuwa wakitumia mchanganyiko uliokuwa na kinyesi cha mwanadamu ili kutibu majeraha.

Je, kuna makosa ya kisayansi katika Biblia?

Mtu anayechunguza Biblia kwa akili iliyofunguka atajibu hapana. Yafuatayo ni maoni fulani yaliyo na kasoro ambayo watu hutoa kuonyesha Biblia si sahihi kisayansi:
Uwongo: Biblia inasema kwamba ulimwengu uliumbwa katika siku sita zenye urefu wa saa 24.
Ukweli: Biblia haitoi tarehe hususa ambayo Mungu aliumba ulimwengu. (Mwanzo 1:1) Pia, siku za uumbaji zinazofafanuliwa katika Mwanzo sura ya 1 ni kipindi cha wakati chenye urefu usiojulikana. Kwa kweli, kipindi chote cha wakati ambacho mbingu na dunia ziliumbwa kinaitwa “siku.”—Mwanzo 2:4.
Uwongo: Biblia inasema kwamba mimea iliumbwa kabla ya jua ambalo husababisha mfumo wa usanidi-mwanga.—Mwanzo 1:11, 16.
Ukweli: Biblia inaonyesha kwamba jua, mojawapo ya nyota zilizo katika “mbingu,” liliumbwa kabla ya mimea. (Mwanzo 1:1) Katika “siku” ya kwanza ya uumbaji, nuru ya jua ilipenya angani na kuanza kuonekana duniani. Anga lilipoendelea kuruhusu mwangaza huo uonekane waziwazi duniani, mfumo wa usanidi-mwanga ulianza kutenda kazi kwenye mimea katika “siku” ya tatu ya uumbaji. (Mwanzo 1:3-5, 12, 13) Baadaye ndipo jua lilipoonekana waziwazi kutoka duniani.—Mwanzo 1:16.
Uwongo: Biblia inasema kwamba jua huzunguka dunia.
Ukweli: Andiko la Mhubiri 1:5 linasema: “Jua limechomoza, na kushuka, nalo linajitahidi kwa nguvu kwenda mahali pake ambapo litachomoza tena.” Maneno hayo yanategemea maoni ya mtu anayetazama jua kutoka duniani. Ni kama vile tu leo tunasema “jua limechomoza” na “jua limetua” hata ingawa ukweli wa mambo ni kwamba dunia ndiyo inayolizunguka jua.
Uwongo: Biblia inasema kwamba dunia ni tambarare.
Ukweli: Biblia inapozungumza kuhusu “miisho ya dunia” inamaanisha “sehemu ya mbali zaidi ya dunia”; maneno hayo hayamaanishi kwamba dunia ni tambarare wala ina mwisho. (Luka 11:31) Vivyo hivyo, maneno “miisho minne ya dunia” ni usemi wa mfano unaorejelea eneo lote la dunia na si kwamba dunia ina pembe nne.—Isaya 11:12; Luka 13:29.
Uwongo: Biblia inasema kwamba mzingo wa mviringo au duara ni mara tatu ya kipenyo chake, lakini hesabu sahihi ni pai (π), au 3.1416 hivi.
Ukweli: Vipimo vinavyotajwa katika 1 Wafalme 7:23 na 2 Mambo ya Nyakati 4:2 vinaonyesha kwamba “Bahari ya kuyeyushwa” ilikuwa na kipenyo cha mikono 10 na kwamba “kamba ya urefu wa mikono 30 ingeweza kuizunguka pande zote.” Huenda vipimo hivyo vilikuwa tu vya kukadiria. Huenda pia mzingo ulipimwa kwa kutegemea sehemu ya nje ya bahari hiyo huku kipenyo kikitegemea upande wake wa ndani.
Posted on : [0] comments Label:

JINSI YA KUWAFUNDISHA WATOTO KUTII

by : Unknown


KIKWAZO

Wewe na mwana wako mwenye umri wa miaka minne mnagombana, na inaonekana kwamba sikuzote mtoto wako hushinda.
  • Unapomwambia afanye jambo fulani anakataa na kukupuuza. *
  • Unapomwambia asifanye jambo fulani analotaka kufanya, hukasirika.
Unajiuliza, ‘Je, hii ni tabia ya kipindi tu? Nitarajie kwamba ataiacha baada ya muda?’
Unaweza kumfundisha mtoto wako kuwa na utii. Hata hivyo, kabla ya kuzungumzia jinsi ya kufanya hivyo, fikiria sababu moja inayomfanya awe na tabia hiyo isiyofaa.

KWA NINI HILO HUTUKIA

Mtoto wako alipokuwa mchanga ulikuwa na wajibu wa kumtunza. Ulimfanyia mtoto jambo lolote alilotaka. Alipolia, ulikuja haraka na kuhakikisha kwamba unampa chochote alichohitaji. Kwa kweli, jambo hilo lilikuwa lenye kufaa na muhimu. Mtoto mchanga huhitaji uangalizi wa wazazi wake daima.
Hata hivyo, baada ya kutendewa hivyo kwa miezi kadhaa, mtoto huanza kutenda kana kwamba ni mkuu wa nyumba na kuwafanya wazazi wake kuwa watumishi walio tayari kutimiza mahitaji yake. Kisha, anapofikisha umri wa miaka miwili hivi, mtoto huyo anagundua ukweli huu wa mambo: “Utawala” wake umeisha. Wazazi wake hawafuati tena maagizo yake; wanatarajia yeye afuate maagizo yao. Hilo linamshtua sana mtoto! Baadhi ya watoto huitikia hali hiyo kwa kukasirika. Wengine hujaribu mamlaka ya wazazi wao kwa kutowatii.
Katika kipindi hicho kigumu, wazazi wanahitaji kudhihirisha wazi mamlaka yao mpya, yaani, kutoa mwongozo ulio wazi wa kile ambacho wanatarajia kutoka kwa mtoto. Lakini, namna gani ikiwa mtoto anapuuza au anakataa mwongozo huo, kama ilivyoonyeshwa katika kisa kilichotangulia?

MAMBO UNAYOWEZA KUFANYA

Ongoza mambo. Mtoto wako hawezi kutii mamlaka yako ikiwa hataona kwamba unaongoza mambo. Hivyo, unahitaji  kuonyesha mamlaka yako kwa usawaziko. Katika miaka iliyopita, baadhi ya watu wanaojiita wataalamu wamedai kwamba neno “mamlaka” lina maana isiyofaa. Mmoja wao hata alidai kwamba mamlaka ya wazazi “haifai” na “hailingani na maadili.” Hata hivyo, ikiwa wazazi watawapa uhuru mwingi, jambo hilo linaweza kuwafanya watoto wakose mwelekeo, wawe walioendekezwa, na wahisi kwamba wana haki ya kupata chochote wanachotaka. Kufanya hivyo hakutamsaidia mtoto kujiandaa na majukumu akiwa mtu mzima.—Kanuni ya Biblia: Methali 29:15.
Toa nidhamu. Kamusi moja inafafanua nidhamu kuwa “mazoezi yanayotokeza utii au kujidhibiti, na mara nyingi adhabu hutolewa sheria zinapovunjwa.” Hata hivyo, nidhamu haipaswi kamwe kuwa yenye kupita kiasi au kwa ukali. Kwa upande mwingine, inapaswa kuwa wazi au inayofaa ili kumsaidia mtoto kujua jambo la kufanyia kazi.—Kanuni ya Biblia: Methali 23:13.
Eleza mambo waziwazi. Baadhi ya wazazi huwaomba tu watoto wao watii. (“Ningependa usafishe chumba chako—Sawa?”) Huenda wazazi wakahisi kwamba hiyo ni njia nzuri. Hata hivyo, mbinu hiyo huenda ikamfanya mzazi asiwe na mamlaka na kumpa mtoto uhuru wa kufikiria faida na hasara za ombi hilo na kisha kuamua iwapo atatii. Badala ya kuacha mamlaka yako, toa mwongozo kwa kueleza mambo waziwazi.—Kanuni ya Biblia: 1 Wakorintho 14:9.
Uwe na msimamo. Ukisema hapana, shikamana na uamuzi huo na hakikisha kwamba wewe na mwenzi wako mnashirikiana. Ikiwa umeamua kutoa nidhamu, shikamana na uamuzi wako. Usijiingize katika makubaliano au mazungumzo ya muda mrefu kuhusu kwa nini ulifanya uamuzi huo. Hivyo itakuwa rahisi sana kwa mtoto wako na kwako, ikiwa ‘utaacha Ndiyo yako imaanishe Ndiyo, na Siyo yako, Siyo.’—Yakobo 5:12.
Uwe mwenye upendo. Familia haipaswi kuongozwa kidemokrasia au kidikteta. Badala yake, ni mpango wa Mungu ambao watoto wanaweza kuongozwa kwa upendo na hivyo kuwa watu wazima wenye kutegemeka. Ikiwa sehemu ya jambo hilo, nidhamu itamfundisha mtoto wako kutii na kumsaidia kuhisi salama chini ya uangalizi wako wenye upendo.

Maelezo ya Chini

^ fu. 5 Ingawa mtoto anayetajwa ni mvulana, kanuni zinazozungumziwa katika makala hii zinawahusu pia wasichana.

Posted on : Tuesday, April 21, 2015 [0] comments Label:

MAHAFALI YA 11 YALIVYOFANA KANISA LA LIVING WATER CENTER MAKUTI - KAWE

by : Unknown
 Jumapili iliyopita yalifanyika mahafali ya 11 ya kozi ya "Life Transforming" katika kanisa la Living Water Makuti Kawe
Kozi hiyo ni ya 11 tangu ianze rasmi mwaka 2004 kanisani hapo
Mahafali hayo yalifanyika kwenye ibada ya jumapili ambayo iliongozwa na mkuu wa kanisa hilo Apostle Onesmo Ndegi (pichani juu) akisaidiwa na mwalimu Lilian Ndegi


Mhitimu akitoa ushuhuda kwenye mahafali hayo
Mhitimu akitoa ushuhuda kwenye mahafali hayo
Mkuu wa kanisa hilo Apostle Onesmo Ndegi akiimba kwa furaha kwenye ibada hiyo pamoja na watendaji wengine wa kanisa hilo


Mwalimu Lilian Ndegi akisema neno kwenye ibada hiyo


Wahitimu wakipokea vyeti vyao kwenye mahafali hayo toka kwa mgeni rasmi ambaye alikua mkuu wa kanisa hilo Apostle Onesmo Ndegi

Picha ya pamoja ya wahitimu na uongozi wa kanisa la Living Water Center - Makuti Kawe
(Picha kwa hisani ya gospel kitaa blog)
Posted on : [0] comments Label:

WAJUA AMRI ZILIZOGAWA MABARA

by : Unknown

Amri Zilizogawa Mabara

Papa Aleksanda wa Sita
BAADA ya Christopher Columbus kurudi kutoka safari yake ya kwanza kuizunguka Amerika katika 1493, wafalme wa Hispania na Ureno walishindwa kukubaliana kuhusu ni nani atakayesimamia biashara na utawala wa kikoloni wa maeneo hayo mapya yaliyogunduliwa. Hispania ilimwomba papa, Aleksanda wa Sita, atatue mgogoro huo.

WAFALME NA MAPAPA WAGAWA MABARA

Hispania, Ureno, na Papa tayari walikuwa wamefikiria kumiliki maeneo mapya yaliyogunduliwa. Katika mwaka wa 1455, Papa Nicholas wa Tano aliipa Ureno haki zote za kuvumbua na kumiliki kila kitu walichopata katika nchi na visiwa vilivyokuwa katika Pwani ya Bahari ya Atlantiki katika Afrika. Kwenye Mkataba wa Alcáçovas wa mwaka wa 1479, Afonso wa Tano wa Ureno na mwana wake, Prince John, walisalimu mamlaka yao juu ya Visiwa vya Canary kwa Ferdinand na Isabella wa Hispania. Ikiwa sehemu ya makubaliano, Hispania ilitambua mamlaka ya Ureno ya kufanya biashara katika Afrika na umiliki wa Azores, Visiwa vya Cape Verde na Madeira. Miaka miwili baadaye, Papa Sixtus wa Nne alithibitisha mkataba huo na kutaja kihususa kwamba ugunduzi wowote mpya katika maeneo ya kusini na mashariki mwa Visiwa vya Canary, ungemilikiwa na Ureno.
Hata hivyo, John, aliyekuwa John wa Pili wa Ureno, alidai kwamba maeneo yaliyogunduliwa na Columbus yalimilikiwa na Ureno. Watawala wa Hispania hawakukubaliana na uamuzi huo, hivyo wakakata rufaa kwa papa mpya, Aleksanda wa Sita, ili awape haki ya kutawala na kuanzisha Ukristo katika maeneo yaliyogunduliwa na Columbus.
Papa Aleksanda wa Sita aligawa mabara kupitia maandishi tu
Ili kusuluhisha hilo, Aleksanda aliweka amri tatu rasmi. Ya kwanza, “kwa mamlaka ya Mungu Mweza-Yote,” aliipa Hispania pendeleo la pekee la umiliki usioisha wa  maeneo mapya yaliyogunduliwa. Amri ya pili iligawanya upande wa kaskazini hadi kusini uliokuwa na urefu wa kilomita 560, magharibi mwa Visiwa vya Cape Verde. Aleksanda alisema kwamba maeneo yoyote yaliyokuwa tayari yamegunduliwa au ambayo yangegunduliwa upande wa magharibi wa mstari huo, yangemilikiwa na Hispania. Papa aligawa mabara kupitia maandishi tu! Amri yake ya tatu iliongezea Hispania umiliki katika upande wa mashariki wa dunia hadi India. Hilo lilimkasirisha sana Mfalme John, ambaye watumishi wake walikuwa wametoka tu kuzunguka kusini mwa Afrika, na hivyo kupanua mamlaka ya Ureno kufikia Bahari ya Hindi.

RAMANI YAGAWANYWA TENA

Akiwa amechoshwa na Aleksanda, * John alifanya makubaliano ya moja kwa moja na Ferdinand na Isabella. Mwandishi William Bernstein anasema hivi: “Watawala wa Hispania walikazia fikira zaidi kumiliki maeneo mapya katika Amerika na pia waliwaogopa sana Wareno waliokuwa wakatili, hivyo walikuwa tayari kufikia makubaliano nao.” Hivyo, mnamo 1494 mkataba ulioitwa Tordesillas ulitiwa sahihi katika mji huo wa Hispania.
Mkataba wa Tordesillas ulidumisha mstari wa upande wa kaskazini hadi kusini uliowekwa na Aleksanda, lakini ukauongeza mpaka kufikia urefu wa kilomita 1,480 zaidi magharibi. Ilidaiwa kwamba bara la Afrika na Asia “yalimilikiwa” na Ureno; na Amerika ilimilikiwa na Hispania. Kuhamishwa huko kwa mstari mpaka upande wa magharibi, kulipanua eneo la utawala wa Ureno mpaka kwenye eneo lililogunduliwa baadaye na kuitwa Brazili.
Amri zilizoipa mamlaka Hispania na Ureno kumiliki na kutetea maeneo mapya waliyopata, zilitumiwa kama msingi wa umwagaji mkubwa wa damu. Amri hizo zilipuuza haki za watu walioishi katika maeneo yaliyogunduliwa kwa kuwakandamiza na kuwatendea isivyo haki. Zimekuwa pia chanzo cha mgogoro wa karne nyingi miongoni mwa mataifa kuhusu umiliki na uhuru wa kutumia bahari.

Maelezo ya Chini

^ fu. 9 Kwa habari zaidi kuhusu papa huyo aliyejulikana kwa kuwa fisadi, tazama makala “Aleksanda wa Sita—Papa Asiyesahauliwa na Roma,” katika gazeti la Mnara wa Mlinzi, Juni 15, 2003, ukurasa 26-29.

by : Unknown

 Kwa nini porojo inadhuru

Porojo fulani hutolewa kwa nia mbaya—kwa mfano, mtu akisema uwongo kimakusudi ili akuchafulie jina. Hata ikiwa mtu anaeneza porojo ambayo haihusu jambo zito, porojo hiyo inaweza kumuumiza mwingine hisia—hasa ikienezwa na mtu uliyemdhania kuwa rafiki yako wa karibu sana!—Zaburi 55:12-14.
“Niligundua kwamba rafiki yangu alikuwa akieneza porojo kunihusu, akisema kwamba mimi siwajali wengine. Jambo hilo liliniumiza sana! Nilishindwa kuelewa kwa nini alisema jambo kama hilo.”—Ashley.
Ukweli wa Mambo: Iwe yule anayeeneza porojo kukuhusu ni rafiki yako au la, haipendezi hata kidogo unapojua kwamba watu wamekuwa wakisema mambo mabaya kukuhusu.

 Jambo baya ni kwamba—huwezi kuzuia porojo

Watu wanaweza kueneza porojo kwa sababu kadhaa, kutia ndani sababu hizi:
Upendezi wa kweli. Wanadamu ni viumbe wanaopenda kuchangamana na wengine. Kwa hiyo ni jambo la kiasili kuzungumza kuhusu kitu au mtu fulani. Biblia yenyewe hututia moyo tuangalie “faida za kibinafsi” za wengine.—Wafilipi 2:4.
“Kwa kawaida, kuzungumza kuhusu watu ndiyo mada inayosisimua zaidi!”—Bianca.
“Lazima nikiri kwamba ninapenda sana kujua mambo ambayo wengine wanafanya na kuzungumzia mambo hayo na watu wengine. Sijui ni kwa nini—inasisimua tu.”—Katie.
Kukosa jambo la kufanya. Katika nyakati za Biblia, kulikuwa na watu ambao “hawakuwa wakitumia wakati wao wa starehe wakifanya chochote ila kuambiana jambo au kusikiliza jambo jipya.” (Matendo 17:21) Hivyo ndivyo ilivyo leo!
“Hata wakati ambapo hakuna lolote la kuchangamsha, watu hubuni jambo fulani ili wawe na kitu cha kuzungumzia.”—Joanna.
Kutojiamini. Biblia ina sababu nzuri ya kutuonya dhidi ya mwelekeo wa kujilinganisha na wengine. (Wagalatia 6:4) Jambo la kusikitisha ni kwamba, watu wengine hukabiliana na tatizo la kutojiamini walilo nalo kwa kueneza habari mbaya kuwahusu wengine.
“Mtu anayeeneza porojo hufunua jambo fulani kuhusu jinsi alivyo. Mara nyingi inafunua kwamba ana wivu na ndio maana anaeneza habari mbaya kuhusu mtu mwingine. Anaeneza porojo hiyo ili tu ajihisi vizuri na ajisadikishie mwenyewe kwamba yeye ni bora kuliko yule mwingine.”—Phil.
Ukweli wa mambo: Upende usipende, watu watazungumza kuhusu watu wengine—kutia ndani wewe.

 Jambo zuri ni kwamba—si lazima porojo ikudhoofishe hisia

Huenda usifaulu kabisa kuwazuia watu kueneza porojo kukuhusu, hata hivyo unaweza kuchagua jinsi utakavyoitikia ukigundua kwamba mtu fulani ameeneza porojo kukuhusu. Ukigundua kwamba habari fulani kukuhusu imeenea, kuna angalau mambo mawili unayoweza kufanya.
JAMBO LA 1: Puuza. Mara nyingi kupuuza jambo fulani ndio uamuzi bora kabisa—hasa ikiwa habari zilizoenezwa ni za upuuzi. Fuata ushauri huu wa Biblia: “Usiwe na haraka kuudhika katika roho yako.”—Mhubiri 7:9.
“Habari zilienea kuwa nilikuwa nikimchumbia mvulana fulani—mtu ambaye hata sikuwahi kukutana naye! Ulikuwa upuuzi mtupu na kwa hiyo niliamua kuupuza.”—Elise.
“Ukiwa na sifa nzuri ni rahisi kwako kukabiliana na porojo. Hata habari mbaya zikienezwa kukuhusu, ni watu wachache watakaoziamini, kwa sababu wanajua kwamba una sifa nzuri. Zitakusaidia uendelee kudumisha hadhi yako.”—Allison.
Dokezo: Andika (1) jambo ambalo lilienezwa kukuhusu na (2) jinsi ulivyohisi. ‘Ukishasema moyoni mwako,’ huenda ukatambua kwamba ni rahisi zaidi kuamua kulipuuza au kulisahau jambo hilo.—Zaburi 4:4.
JAMBO LA 2: Mfikie mtu aliyeanzisha porojo hiyo. Katika visa fulani huenda ukahisi kwamba habari mbaya sana kukuhusu imeenezwa hivi kwamba ukaamua kuchukua hatua ya kumfikia yule aliyeianzisha.
“Unapowafikia watu wanaoeneza porojo kukuhusu, huenda ukawasaidia watambue kwamba hatimaye mambo wanayosema humfikia mtu wanayeeneza habari zake. Hilo huenda likakusaidia ujisafishie jina au hata kusuluhisha tatizo lenyewe.”—Elise.
Kabla ya kumfikia mtu anayeeneza porojo kukuhusu, fikiria kanuni zifuatazo za Biblia na ujiulize maswali yaliyoambatanishwa na kanuni hizo.
  • “Yeyote anapojibu jambo kabla ya kulisikia, huo ni upumbavu na aibu kwake.” (Methali 18:13) ‘Je, nina habari zote zinazohusika? Je, inawezekana kwamba mtu aliyeniletea porojo hizo hakuelewa vizuri mambo aliyosikia?’
  • ‘Uwe mwepesi wa kusikia, si mwepesi wa kusema, si mwepesi wa ghadhabu.’ (Yakobo 1:19) ‘Je, huu ndio wakati unaofaa wa kumfikia mtu anayeeneza porojo kunihusu? Je, nina uhakika kwamba ninatumia njia inayofaa kusuluhisha jambo hilo? Au ni afadhali zaidi nisubiri wakati fulani upite ili hisia zangu zitulie?’
  • “Chochote ambacho mngetaka mtendewe na watu, ninyi nanyi watendeeni vivyo hivyo.” (Mathayo 7:12, Holy Bible) ‘Ikiwa ningekuwa nimeeneza porojo kumhusu mtu mwingine, ningetaka mtu huyo anifikie kwa njia gani? Ningependa tuzungumzie tatizo hilo chini ya hali gani? Ningependa atumie maneno ya aina gani na azungumze kwa njia gani?’
Dokezo: Kabla ya kumfikia yule anayeeneza porojo kukuhusu, andika mambo utakayomwambia. Kisha subiri juma moja au mawili, halafu urudie mambo uliyoandika uone kama kuna mabadiliko yoyote unayohitaji kufanya. Kisha zungumzia mambo hayo na mzazi wako au rafiki mkomavu na umwombe mashauri.
Ukweli wa mambo: Kama ilivyo na mambo mengi maishani, huwezi kuwazuia watu wasieneze porojo. Lakini hilo halimaanishi kwamba ni lazima porojo ikudhibiti!

(Source:www.jw.org)