Dar es Salaam. Askofu Dk Fredrick Shoo amechaguliwa kuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), akichukua nafasi ya Dk Alex Malasusa aliyemaliza kipindi chake cha miaka minane.
Dk Shoo, ambaye pia ni askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, alichaguliwa juzi usiku katika siku ya tatu na ya mwisho ya mkutano mkuu wa 19 wa kanisa hilo uliofanyika Chuo Kikuu cha Tumaini (Tuma) jijini Arusha baada ya kuwashinda maaskofu wenzake wawili, katika uchaguzi uliokuwa na kila aina ya ushindani.
Waliokuwa wakichuana kuwania nafasi hiyo baada ya kupendekezwa na Halmashauri Kuu ya KKKT ni Askofu Dk Stephen Munga wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Askofu Charles Mjema wa Dayosisi ya Pare na Dk Shoo.
Mwenyekiti wa uchaguzi huo, Dk Malasusa, ambaye pia ni askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, alimtangaza Dk Shoo kuwa mkuu wa kanisa hilo kwa kipindi cha miaka minne baada ya kupata kura 153, huku Dk Munga akipata kura 67, ikiwa ni baada ya uchaguzi huo kurudiwa mara tatu kutokana na mshindi kutopata zaidi ya theluthi mbili ya kura zote.
Kanuni za uchaguzi za KKKT zinaeleza kuwa mshindi atapatikana kwa kupata kura zisizopungua theluthi mbili ya kura zote zilizopigwa, iwapo mshindi hatapatikana katika duru la kwanza, majina mawili yaliyopata kura nyingi ndiyo yatakayopigiwa tena kura.
Iwapo theluthi mbili haitapatikana katika duru la pili, kura ya wingi au uchache itatumika kwa duru la tatu ili kumpata mshindi.
Katika kuhakikisha mshindi anapatikana, mkutano huo ulilazimika kutumia hatua ya wingi wa kura na Dk Shoo kuibuka mshindi.
Katika awamu ya kwanza, Askofu Mjema alipata kura 53, Dk Munga kura 81 na Dk Shoo kura 86, idadi ambayo haikufika theluthi mbili ya kura zote kulingana na kanuni za kanisa hilo jambo lililosababisha uchaguzi kurudiwa mara ya pili.
Dk Malasusa alitangaza matokeo ya awamu ya pili ya kura zilizopigwa ambapo Askofu Munga alipata kura 94 na Dk Shoo kura 124. Kura moja ikiharibika.
Kabla ya kuanza kwa mkutano huo wajumbe wa Halmashauri Kuu walipitisha majina matatu ya maaskofu waliowania nafasi hiyo na kuyapeleka kwenye mkutano huo ili yapigiwe kura.
Wajumbe wa mkutano huo mara baada ya kupewa karatasi za kupigia kura walikwenda katika vyumba maalum kwa ajili ya kumchagua askofu wanayemtaka, mara baada ya kuchagua walitakiwa kurejea ukumbini na kutumbukiza karatasi hizo katika vifaa vilivyoandaliwa kuhifadhia kura hizo.
Kauli ya Dk Shoo
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Dk Shoo alimshukuru Mungu huku akionyesha mshangao wa kuchaguliwa kwake.
“Sijui nimepataje nafasi hii, ni nguvu ya Mungu tu kwa kweli. Kwa ushirikiano wa waumumini wote nitaweza kufanya kazi hii, naomba mniombee,” alisema.
Alichokisema Malasusa
Akizungumza katika ibada ya kufunga mkutano huo uliomalizika saa 6:00 usiku, Dk Malasusa alisema anamuachia madaraka Dk Shoo katika hali ya amani na utulivu, huku akiwapongeza viongozi na maaskofu wote wa kanisa hilo.
Awali kabla ya kuanza kwa uchaguzi huo, mkutano huo ulimchagua Alice Mtui wa Dayosisi ya Konde kuwa mwandishi wa kanisa hilo kwa kipindi cha miaka minne.
Alice alipigiwa kura 201 na wajumbe wa mkutano huo, huku kura za hapana zikiwa 17 na kura moja ikiharibika.
(Chanzo: Mwananchi Communications)